WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Bunge la
Afrika Mheshimiwa Stephen Masele na kumuahidi kwamba Serikali itampa
ushirikiano ili aweze kutimiza majukumu yake.
Ametoa
ahadi hiyo leo (Jumanne, Juni 5, 2018) wakati akizungumza na Mheshimiwa
Masele ofisini kwake Bungeni, Dodoma. Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kumpongeza kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Amesema
ushindi wake katika nafasi hiyo umelipa heshima kubwa Bunge na Serikali
na kwamba wana matarajio makubwa kwa sababu uwepo wake, utaliongezea
Taifa ushirikiano na nchi nyingine za Afrika.
"Matarajio
kwa Bunge ni makubwa kwani kuna mambo ambayo tunataka ushirikiano na
nchi nyingine za Afrika, hivyo uwepo wako ni muhimu katika kufanikisha
utekelezaji wake."
Vilevile,
Waziri Mkuu amewapongeza wabunge wengine wawili, Waheshimiwa David
Silinde na Asha Abdullah Juma kwa ushirikiano wao uliochangia ushindi wa
Mheshimiwa Masele.
Kwa
upande wake, Mheshimiwa Masele ambaye ni Mbunge wa Shinyanga Mjini,
ameishukuru Serikali kwa ushirikiano iliyompa na hatimaye kuibuka na
ushindi huo.
Amesema
ushindani ulikuwa mkali kutokana na uwepo wa mataifa mengi yaliyokuwa
yakiwania nafasi hiyo. Aliahidi kutetea maslahi ya Taifa kwa muda wote
atakaotumikia nafasi hiyo. “Nakuhakikishia Waziri Mkuu kwamba
nitayalinda na kuyatetea maslahi ya Tanzania kwa muda wote ambao
nitakuwa katika wadhifa huu,” alisema Mhe. Masele.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Chapisha Maoni