ENEO
lililokuwa limetengwa ili ijengwe Ikulu ndogo ya Mkoa wa Mbeya
limemegwa na kuuzwa. Limeuzwa kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni
maofisa wa ardhi Jiji la Mbeya, kutumia fursa ya eneo hilo kujinufaisha
kwa kuuza viwanja.
Inaelezwa
kuwa baadhi ya maofisa ardhi wa halmashauri ya jiji, wamepima viwanja
kwenye eneo hilo wakishirikiana na wakazi ambao ilikuwa walipwe fidia
kwa mashamba yao, na wakazi hao wanatumiwa kutafuta wateja wa viwanja
hivyo ili ionekane wao ndiyo walioviuza kwa watu wanaojenga sasa.
Mkuu
wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla jana alitembelea eneo hilo lililopo Veta
jijini Mbeya na kujionea majengo yaliyojengwa kwenye ardhi, iliyokuwa
sehemu ya uwanja wa kujengwa Ikulu ndogo ya Mkoa.
Diwani
wa Kata ya Ilomba, Dickson Mwakilasa alimwambia Mkuu wa Mkoa kuwa eneo
lilikojengwa nyumba za watu binafsi, lilikuwa la serikali na
kilichotakiwa ni kulipa fidia kwa wakazi waliokuwa na mashamba maeneo ya
jirani.
Kufuatia
hali hiyo, Makalla alilazimika kuwahoji maofisa wa halmashauri ya jiji,
lakini wote wakaonekana kutoijua vyema historia ya eneo hilo, hivyo
ikamlazimu Mkuu huyo wa Mkoa kuahidi kufuatilia kwa haraka nyaraka
husika.
Alisema
anachotaka kujua ni ramani inayoonesha ukubwa wa eneo la awali; na pia
matumizi yaliyopangwa, huku akisema anachojua yeye mpaka sasa ni kuwa
maofisa ardhi wameuza kinyemela sehemu ya uwanja wa Ikulu ya Mkoa.