Mwanasiasa
mkongwe na Mwenyekiti wa Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP),
Augustine Mrema ameweka wazi jinsi timu yake ilivyowahi kufoji sakata la
ufisadi dhidi ya Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Mheshimiwa
Benjamin Mkapa, kwa lengo la kujipatia umaarufu.
Akizungumza
leo kwenye mahojiano na kipindi cha Maisha Mseto cha Times FM, Mrema
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, amesema kuwa kuna
wakati vyama vya upinzani kwa lengo la kujipatia umaarufu, hutunga
kashfa dhidi ya Serikali na viongozi wake kama yeye na timu yake
walivyowahi kufanya miaka ya 1990.
Mwanasiasa
huyo alisema kuwa anakumbuka mwaka mmoja baada ya kutoka kwenye
uchaguzi, walifoji barua na kutunga dhidi ya Serikali kuwa viongozi wa
juu na hadi kumtaja Mheshimiwa Mkapa kuwa alifanya ufisadi wa sh.900
milioni.
“Lile
tukio la Mh. Mkapa kwamba amekula Milioni 900, tulitengeneza sisi ili
kumnyima sifa Mheshimiwa Mkapa na wananchi watuamini sisi watupe
nafasi,” alisema.
Alifafanua
kuwa timu yake kwa pamoja walikubaliana kuwa kwakuwa yeye ndiye
aliyekuwa na ushawishi zaidi kwa wananchi alibebe sakata hilo ‘feki’ na
alifanya hivyo; alisema “tulipanda kwenye majukwaa na barua ile ya
kufoji na tukawa tunahoji kuhusu fedha zile.”
Mwanasiasa
huyo ambaye miaka ya 1990 alikuwa kiongozi wa upinzani mwenye ushawishi
mkubwa zaidi akigombea urais tangu mwaka 1995, alisema kuwa hadi sasa
baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikitunga matukio ya kuichafua
Serikali na hata Rais kwa lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa.
Wakati huo, Mrema alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, chama ambacho kilikuwa chama kikuu cha upinzani.
Katika
hatua nyingine, Mrema alisifu kazi inayofanywa na Rais John Magufuli na
kueleza kuwa ndani ya muda mfupi Serikali yake imefanikiwa kupambana na
ufisadi kwa kiasi kikubwa.
Alisema
alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alijaribu kupambana na
ufisadi, hali iliyosababisha achukiwe na wengi, lakini hakufanikiwa kama
alivyofanikiwa Rais Magufuli.
“Unajua
ili ufanikiwe kwa baadhi ya mambo ya nchi ni lazima uwe Rais kwakuwa
unakuwa wewe ndiye muamuzi wa mwisho. Mimi nilishindwa kwa sababu wakati
mwingine unakuwa unafanya jambo lakini lisipoungwa mkono na walio juu
yako huwezi kufanikiwa,” alisema.
“Sasa
hivi mwenye nchi ndiye anayepambana na ufisadi. Atafanikiwa kwa sababu
yeye ndiye anayesimamia kuliko wakati wangu mimi sikuwa na Serikali,”
Mrema aliongeza na kutoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu na
kumsikiliza Rais John Magufuli.
Akizungumzia
mpango wa kugombea ubunge katika jimbo la Vunjo kwenye uchaguzi wa
mwaka 2020, Mrema alisema atawasikiliza wananchi wa jimbo hilo ambao
amedai wanalalamika kwa kukosa maendeleo baada ya kutomchagua.
Mrema
alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 alipokuwa akitetea kiti chake
cha ubunge wa Vunjo na nafasi yake ikachukuliwa na Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia kupitia Ukawa.
0 comments:
Chapisha Maoni