Waziri
wa Mambo ya Nje, Augustine Mahiga atafanya ziara ya kikazi nchini
Israel kuanzia kesho Mei 7, 2018 hadi Mei 10, 2018, ziara inayotokana na
mwaliko wa Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Benjamin
Netanyahu.
Atakapowasili
nchini humo, Dk Mahiga atafanya mazungumzo na Netanyahu na kushiriki
uzinduzi wa ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Israel.
Taarifa
ya Wizara ya Mambo ya Nje iliyotolewa leo Mei 6, 2018 imesema Dk Mahiga
anakuwa waziri wa kwanza wa Mambo ya Nje kutoka Tanzania kufanya ziara
nchini Israel.
Mbali
ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, Waziri
Mahiga atatumia ziara hiyo kuishawishi Serikali ya Israel iunge mkono
juhudi za Serikali za kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda.
Israel
ni moja ya nchi zenye maendeleo makubwa katika sekta za kilimo,
viwanda, uhifadhi wa maji, matibabu, ulinzi na usalama, mawasiliano na
nishati ya joto ardhi.
“Kupitia
ziara hiyo, ajenda ya uchumi wa viwanda ya Tanzania inaweza kupata
ushirikiano mkubwa wa Israel kutokana na hatua kubwa ya kimaendeleo
iliyofikia,” inasema taarifa ya wizara.
Kabla
ya Tanzania kufungua ofisi ya ubalozi Israel, ilikuwa inawakilishwa
kupitia ubalozi wa Misri na ubalozi wa Israel nchini Kenya pia
unawakilisha Tanzania hadi sasa.
Israel
ni moja kati ya nchi sita ambazo Serikali ya Tanzania imefungua balozi
mpya. Job Masima aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa balozi wa kwanza
wa Tanzania nchini Israel.
0 comments:
Chapisha Maoni