Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imechukua fedha zote zilizokuwapo katika
akaunti ya kampuni ya StarTimes Tanzania kufidia deni la kodi.
Kampuni
ya StarTimes iliyoleta mapinduzi ya matangazo ya digitali nchini tangu
kuzimwa kwa mitambo ya analogia kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka
2012, inajishughulisha na uuzaji wa ving’amuzi na vifurushi vyake, simu
za mkononi na runinga.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema jana
kwamba mamlaka hiyo imezuia akaunti ya StarTimes kwa sababu ya kushindwa
kulipa kodi kwa wakati.
Kayombo alisema akaunti hiyo ilizuiwa kwa siku tatu kabla ya kufunguliwa.
“Ukiona
mpaka tumefikia hatua hii ujue suala hilo lilikuwa sugu, hivyo tuliamua
kuzuia kwa muda wa siku kama mbili au tatu hivi ili kuhakikisha fedha
inapatikana,” alisema.
Kayombo
alisema, “Hatukuifungia ila tuliizuia kwani operesheni zake za kuweka
ziliendelea kama kawaida, kwa maana ya kuweka fedha isipokuwa walikuwa
hawawezi kutoa, lakini sasa tumewafungulia.”
Alisema baada ya siku tatu, mamlaka hiyo ilichukua fedha zote zilizokuwapo na kuiachia akaunti hiyo.
“Katika
akaunti tulikuta fedha kiasi lakini pia kwa muda tuliyoizuia kuna
nyingine ziliingia, hivyo ilibidi tuchukue zote ili kulipa deni hilo,”
alisema.
Hata
hivyo, alisema fedha hizo bado hazitoshi kumaliza deni, na kueleza kuwa
ni lazima kampuni hiyo ilipe ili kujiweka katika mazingira mazuri ya
kufanya biashara.
Alipoulizwa
kiasi cha deni inachodai na kilichosalia, Kayombo alisema hiyo ni siri
kati ya mamlaka na mteja wake na anayepaswa kutaja kiasi ni mteja.
“Sheria
inatukataza kutaja kiasi tunachodai lakini ninachoweza kusema tu kwa
sasa ni kweli tumechukua fedha zote baada ya kuzuia akaunti kwa
kushindwa kulipa kodi kwa wakati,” alisema.
Alipoulizwa
iwapo mamlaka imetoa muda kwa kampuni hiyo kulipa deni lililobaki,
Kayombo alisema, “Sheria ya kodi inataka mtu kulipa kodi yake kwa wakati
na si vinginevyo.”
Alisema,
“Kama wana sababu ya msingi ya kutaka kuongezwa muda, milango yetu ipo
wazi, wafuate taratibu na kuja kuzungumza na kamishna wa kodi.”
Awali,
ilielezwa kwamba kwa muda mrefu, StarTimes imekuwa ikisuasua katika
ulipaji kodi jambo lililosababisha kuonywa mara kadhaa na TRA.
0 comments:
Chapisha Maoni