Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Kwa
mara ya kwanza katika historia ya nchi, Serikali imezindua Mkakati wa
kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi yenye
kuchochea upatikanaji wa mapato ili ziweze kujitegemea.
Mkakati
huo umezinduliwa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Ashatu Kijaji, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango, ambapo amesema kiasi cha shilingi bilioni 131.47 kitatumika
kutoa ruzuku ya utekelezaji wa miradi 22 kwa halmashari 17 zilizoko
katika mikoa 10 nchini, katika mwaka wa fedha 2018/19.
Ameitaja
mikoa hiyo ambayo Halmashauri zake zimekidhi vigezo vya kunufaika na
miradi ya kimkakati katika awamu ya kwanza ya mpango huo kuwa ni Dar es
Salaam, Geita, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Morogoro, Mtwara, Pwani,
Simiyu na Songwe.
Amesema
kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Halmashuri zinajenga uwezo
wa kujitegemea kwa takribani asilimia 80 hadi 100 ifikapo mwaka 2025,
badala ya hali ya sasa ambapo halmashauri hizo zinategemea ruzuku kutoka
Serikali Kuu kwa zaidi ya asilimia 88.
Amezitaka
halmashuri zitakazopata fedha za miradi hiyo kuhakikisha fedha hizo
zinawekezwa kwenye miradi yenye tija, inayokuza ajira kwa wananchi na
kuongeza mapato ya halmashauri.
Ametoa
wito kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri kubuni miradi
ya kibiashara kwa ajili ya wananchi wanaowaongoza kwa kutengeneza ajira
kwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Alionya
kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watendaji wanaosimamia
miradi hiyo ikiwa watatumia fedha hizo kwa malengo tofauti na
yaliyokusudiwa na kurejea kauli ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwamba
kufuja fedha za Serikali katika kipindi hiki ni sawa na kunywa sumu.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James,
amesema kuwa Serikali inazo fedha za kutosha kufanikisha mkakati huo na
kutoa wito kwa viongozi wa Mikoa husika kuchangamkia fursa hiyo kwa
kuanisha miradi yenye tija ili ipatiwe fedha.
Alifafanua
kuwa tayari Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 15 kwa ajili
ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika mkoa wa Dar es
Salaam katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kujenga Kituo
cha Mabasi cha Mbezi Luis, Ujenzi wa Soko la Mburahati katika Manispaa
ya Ubungo, Ujenzi wa Soko la Kisasa la Magomeni katika Manispaa ya
Kinondoni na Ujenzi wa Soko la Kisasa la Kisutu, Ujenzi wa Machinjio ya
Kisasa ya Vingunguti katika Manispaa ya Ilala.
Naye
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-
TAMISEMI Selemani Jaffo (Mb) amesema kuwa Ofisi yake itaanza kufuatilia
na kupima utendaji kazi wa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ili
kuona kama wanaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliwapongeza
Wakurugenzi walioonesha mfano katika kuendana na kasi ya Serikali ya
Awamu ya Tano kwa kubuni miradi yenye tija na ya kimkakati iliyopewa
Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango na kuwataka watendaji wengine waige
mfano huo.
Baadhi
ya miradi itakaotekelezwa na Halmashauri zilizokidhi vigezo ni pamoja
na Ujenzi wa Masoko ya Kisasa, Ujenzi wa Maegesho ya Malori, Ujenzi wa
stendi za kisasa, Maghala ya kuhifadhi mazao, Masoko ya Kisasa,
Machinjio na Ujenzi wa Viwanda.
0 comments:
Chapisha Maoni