Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
SERIKALI
imeitaka Sekta ndogo ya Benki kuongeza ubunifu kwa kutoa mikopo ya muda
mfupi na mrefu ambayo itawezesha ukuaji wa sekta za viwanda na kilimo
pamoja na wajasiriamali wadogo.
Hayo
yamebainishwa Jijini Dodoma na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
Prof. Florens Luoga, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip
Mpango, katika Mkutano wa wadau wa Sekta ya Fedha uliowashirikisha
wabunge, washirika wa Maendeleo, wakuu wa Taasisi za fedha na Wizara ya
Fedha na Mipango.
Prof.
Luoga alitoa wito huo kufuatia kuwepo kwa changamoto katika Sekta hiyo
ikiwemo ukosefu wa uwekezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika
viwanda, kilimo na miundombinu pia ukosefu wa mikopo kwa wajasiriamali
wadogo na wa kati.
“Kuna
kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma za bima za kilimo, gharama
kubwa za huduma za fedha, mifumo hafifu ya kuwalinda watumiaji wa
huduma za fedha, ukosefu wa elimu ya fedha kwa wananchi na wananchi
wengi kutofikiwa na huduma za fedha ambapo ni asilimia 8.6 tu ya nguvu
kazi ya wananchi waishio vijijini wanapata huduma za benki
ikilinganishwa na asilimia 32.1 ya nguvu kazi kwa wanaoishi mijini”
alisisitiza Prof Luoga
Gavana
huyo wa Benki Kuu alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo,
Serikali ilifanya maboresho ya Sekta ya Fedha katika eneo la
ubinafsishaji wa benki za Serikali kurekebisha na kutunga sera na sheria
mbalimbali hadi kufikia Desemba, 2017 ili kuweka misingi imara ya
kuwezesha ukuaji, ushindani na ufanisi katika sekta ya fedha.
“Maboresho
ya Sekta ya Fedha yamesaidia ongezeko la idadi ya benki na taasisi za
fedha kufikia 54, kampuni za bima 31, kampuni zilizoorodheshwa kwenye
soko la hisa 27, taasisi za huduma ndogo za fedha takriban 450, mifuko
na program za Serikali 34, vikundi vya kifedha vya kijamii takribani
30,019 katika mikoa 18 ya Tanzania bara na uanzishwaji wa soko la
bidhaa” alieleza Prof. Luoga.
Alisisitiza
kuwa taasisi za fedha zikitimiza wajibu wake, sekta binafsi itakuwa na
uwezo wa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa viwanda, kuongeza
uzalishaji wa bidhaa zitakazouzwa nje ya nchi na hatimaye kukuza uchumi
wa Taifa na kupunguza umasikini wa kipato wa wananchi.
Aidha
Serikali katika kupunguza umaskini na kukuza uchumi, inaandaa Mpango
Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha, unalenga kuongeza upatikanaji wa
huduma jumuishi za fedha, kulinda watumiaji wa huduma za fedha,
upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, uthabiti wa sekta ya fedha,
kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha,
kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu na kuweka mazingira wezeshi ya
sheria, kanuni na taratibu katika sekta hiyo.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu,
akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Doto James,
alisema kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha uchumi wa
nchi unaongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Kuwepo
kwa viwanda vingi italeta ongezeko la ajira kwa wananchi walio wengi
pamoja na kuiongezea Serikali mapato” alieleza Dkt. Kazungu
Aidha,
kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuwekeza katika viwanda vidogo
vidogo, ni lazima wapate rasilimali fedha kutoka kwenye taasisi kama
vile benki na masoko ya mitaji hivyo watoa huduma kwenye taasisi hizo
wanapaswa kuongeza ubunifu kwenye utoaji wa huduma zinazokidhi mahitaji
ya wapokeaji huduma kulingana na shughuli wanazofanya na kwa gharama
nafuu.
Alizitaka
taasisi za fedha kuwekeza katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa
kutumia taasisi hizo kwa kujiwekea akiba na kupata mitaji itakayowezesha
kukuza biashara na shughuli zao za kiuchumi hivyo wadau wa sekta ya
fedha wanapaswa kujiuliza ni kwa nini mikopo ya biashara kwenda kwenye
sekta binafsi hairidhishi.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Prof.
Faustin Kamuzora aliwataka wadau wa sekta ya fedha kuzungumzia mafanikio
ya Sekta ya fedha kwa njia ya miamala ya Simu za mkononi kwa kuwa
Tanzania imepiga hatua kubwa Duniani katika eneo hilo na hivyo kuwa
mfano kwa mataifa mbalimbali.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante
Ole Gabriel ameitaka Sekta binafsi inayonufaika na mikopo inayotolewa na
taasisi za fedha kuwekeza kwenye miradi yenye tija na kulipa mikopo yao
kwa wakati pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha na
kuongeza kiwango cha mauzo ya bidhaa hizo nje ya nchi,
mwisho
0 comments:
Chapisha Maoni