Wabunge
wawili wa Chadema leo Mei 17, 2018 wamejikuta njia panda baada ya Naibu
Spika, Dk Tulia Ackson kumzuia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kujibu
maswali yao kwa madai kuwa si ya kisera.
Waliomuuliza
Waziri Mkuu maswali bungeni leo katika kipindi cha maswali ya papo kwa
hapo kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni ni mbunge wa
Tunduma, Frank Mwakajoka , Pauline Gekul (Babati Mjini).
Gekul
alimuuliza Waziri Mkuu kuhusu sera ya Serikali ya mwaka 1996 ya
kushusha madaraka katika halmashauri na lengo likiwa ni kuzipa
halmashauri nguvu, kubuni vyanzo vya mapato na kutumia.
“Stendi
ya mabasi ya babati ilipokonywa kwa madai kuwa ni agizo la Rais na Rais
amesema hahusiki bali ni viongozi wa Manyara, nini kauli ya serikali,”
amehoji Gekul.
Baada ya swali hilo, Dk Tulia amesema si la kisera na linaweza kujibiwa na waziri hivyo kumtaka kukaa na kutafuta swali jingine.
Hata
pale Gekul alipopewa fursa ya kuuliza jingine bado amesema ,”ni swali
la kisera, “ jambo lililomfanya Dk Tulia kumtaka aketi.
Kwa
upande wake Mwakajoka amesema kumekuwa na migogoro katika halmashauri
mbalimbali nchini kati ya wakuu wa wilaya na madiwani, kutolea mfano
Gairo, Malinyi na Mbeya Mjini.
Amesema
katika Halmashauri ya Tunduma kuna mgogoro ambao umesababisha baraza la
madiwani kutokaa kikao tangu Agosti 2017, kwamba licha ya maelekezo
kadhaa ya waziri ila mkuu wa mkoa na wilaya wanagoma kufanyika kwa kikao
hicho.
Kama ilivyokuwa kwa Gekul, Dk Tulia pia alipangua swali hilo na kubainisha kuwa linaweza kujibiwa na waziri mwenye dhamana.
Mara
baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Gekul amesimama
kuomba mwongozo akitumia kanuni ya 68(7) akizungumzia swali lake
lilizozuiwa akisema ni swali la kisera, “Lakini lina maslahi kwa umma
kwa watu wa Babati na Naibu Spika hili swali limekwisha kufikishwa kwa
Waziri Mkuu na nyaraka tulishampatia, hili jambo limekuwa likisingiziwa
Rais.”
“Waziri
Mkuu ni msimamizi wa shughuli za Serikali na Rais kajivua hahusiki na
mimi nimeuliza, nashindwa kuelewa, wabunge wengine wanauliza suala la
jimboni na anajibiwa, nikuombe mwongozo wako, suala hili litaendelea
hadi lini na suala la dhuruma mwisho hukurudia. Kwa nini meza isimwache
waziri mkuu ajibu maswali yetu badala ya kumchagulia?”
Akijibu
mwongozo huo, Dk Tulia amesema utaratibu waliojiwekea, kwamba maswali
atakayoulizwa Waziri Mkuu yana utaratibu wake na ya mawaziri yana nafasi
yake, “kama waziri mkuu analijua au halijui hilo si lenye mamlaka
yangu.”
“Maswali
ya majimbo yanaulizwa kwa mawaziri, maswali ya kisera ambayo mawaziri
hawawezi kujibu ndio anaulizwa Waziri Mkuu. Kanuni zetu zimesema wazi
maswali ya kisera au ya kijamii, kijamii si barabara ya jimbo lako.”
Amesisitiza,
“ Si swali la Gekul pekee hata la Mwakajoka limezuiwa, swali la Tunduma
waziri mkuu analijuaje. Niwasihi maswali kwa Waziri Mkuu tujielekeze
katika maswali ya kisera.”
0 comments:
Chapisha Maoni