WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza
kaulimbiu yake ya kujenga uchumi unaotegemea viwanda na kwamba hadi
kufikia Februari 2018, viwanda vipya 3,306 vimekwishaanzishwa nchini.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati
akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa
mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019
kwenye mkutano wa 11 wa Bunge.
Amesema
Serikali inahamasisha uwekezaji katika viwanda kwa kutoa vivutio vya
kodi na visivyo vya kodi kwa wawekezaji mahiri (strategic investors);
kuendeleza na kuboresha miundombimu wezeshi kama vile barabara, reli,
bandari, umeme na maji. “Serikali itaendelea kuhuisha sera, sheria na
kanuni pamoja na kufuatilia utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa na
kuchukua hatua stahiki kwa wamiliki walioenda kinyume na mikataba ya
mauzo,” amesema.
Waziri
Mkuu amelieleza Bunge kwamba mikoa na Halmashauri zote nchini
zimeelekezwa kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya viwanda na kwamba
katika mwaka 2018/2019, Serikali itatoa kipaumbele katika kutekeleza
miradi ya kielelezo, uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi pamoja na
kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji katika sekta ya
viwanda.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu ushiriki wa sekta ya hifadhi ya jamii kwenye ujenzi wa
uchumi wa viwanda, Waziri Mkuu amesema pamoja na miradi mingine NSSF na
PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wanatekeleza mradi mkubwa wa
uzalishaji wa sukari mkoani Morogoro.
“Lengo
la mradi huo ni kuzalisha tani 250,000 za sukari na umeme megawati 40.
Mradi huo unatekelezwa katika shamba la Mkulazi lililopo Ngerengere
lenye ukubwa wa hekta 63,000 na shamba la gereza la Mbigiri lenye ukubwa
wa ekari 12,000 lililopo Dakawa,” alisema.
“Hadi
sasa ekari 2,000 za mashamba ya miwa zimetayarishwa katika eneo la
Mkulazi na ekari 1,100 zimepandwa miwa. Lengo la Serikali ni kukamilisha
awamu ya kwanza ya ufungaji wa mitambo ya kiwanda cha Mbigiri ifikapo
mwezi Desemba, 2018 ili uzalishaji uanze mwaka 2019,” alisema na
kuongeza kuwa miradi hiyo itakapokamilika, itazalisha zaidi ya ajira
100,000.
Waziri
Mkuu alisema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo Juni 2017, ajira
za moja kwa moja 780 na ajira zisizo za moja kwa moja 24,000
ikijumuisha wakulima wadogo wa mbegu na kilimo cha nje zimezalishwa.
Akifafanua
kuhusu ujenzi wa barabara kuu, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea
kuboresha mtandao wa barabara nchini ambapo katika kipindi cha Julai
2017 hadi Februari 2018, ujenzi wa Km. 776.45 za barabara kuu kwa
kiwango cha lami umekamilika na Km. 1,760 zinaendelea kujengwa. Pia
barabara zenye urefu wa Km. 17,054 zilikarabatiwa katika kipindi hicho.
Kuhusu
ujenzi wa madaraja, Waziri Mkuu alisema madaraja ya Kilombero na Kavuu
ujenzi wake umekamilika na kwamba ujenzi unaoendelea hivi sasa ni wa
madaraja ya Sibiti, Mto Mara, Lukuledi, Ruhuhu, Momba na Mlalakuwa.
Alisema madaraja mengine 996 katika maeneo mbalimbali nchini
yamekarabatiwa.
Kuhusu
jitihada za Serikali kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar
es Salaam, Waziri Mkuu alisema hadi kufikia Februari 2018, ujenzi wa
barabara ya juu katika eneo la TAZARA ulikuwa umefikia asilimia 70 na
ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo (Ubungo Interchange)
umeanza.
“Maandalizi
ya awamu ya pili hadi ya nne ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya
mabasi yaendayo haraka yanaendelea. Katika mwaka 2018/2019, Serikali
imepanga kujenga kilometa 597 za barabara kuu na za mikoa kwa kiwango
cha lami na kilometa 72 za kiwango cha lami zitakarabatiwa,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuliarifu Bunge juu ya
uanzishwaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tanzania Rural
and Urban Roads Agency – TARURA) kwa lengo la kurahisisha huduma za
usafirishaji na kuongeza kasi ya wananchi kujiletea maendeleo.
Alisema
TARURA imepewa jukumu la kusimamia ujenzi na matengenezo ya mtandao wa
barabara zenye urefu wa kilometa 108,946.2 za vijijini na mijini.
“Katika mwaka 2017/2018, TARURA imesimamia matengenezo ya barabara zenye
urefu wa kilomita 4,183.3, madaraja 35, makalavati makubwa 43 na madogo
364 na drift nne,” alisema.
Waziri
Mkuu aliliomba Bunge likubali kupitisha sh. 143,618,762,698 zikiwa ni
makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2018/2019
ambapo sh. 74,527,321,698 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh.
69,091,441,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile,
Waziri Mkuu aliliomba Bunge liidhinishe sh. 125,521,100,000 kwa ajili
ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 117,205,487,000 ni kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na sh. 8,315,613,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO, APRILI 4, 2018
0 comments:
Chapisha Maoni