WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha vyama vya
msingi vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha mazao
ya kimkakati ya biashara ya pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku.
Amesema
katika mwaka 2018/2019, Serikali inalenga kuimarisha masoko ya mazao
hayo kwa kuhamasisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo mazao hayo
yatazalishwa na kuuzwa kupitia vyama vya ushirika kwa njia ya minada.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati
akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa
mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019
kwenye mkutano wa 11 wa Bunge.
Waziri
Mkuu amesema pamoja na hatua hizo, Soko la Bidhaa ambalo
limeshaanzishwa, litasaidia sana kuimarisha masoko ya mazao kwani
yatakuwa yanauzwa kwa njia ya ushindani mkubwa huku wakulima
wanaozalisha kwa ubora wakinufaika na bei ya juu zaidi.
“Serikali
imeamua kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao matano ya
biashara ambayo ni chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku. Lengo ni
kuongeza mapato ya wakulima, kuwa chanzo cha kuaminika cha malighafi
katika uchumi wa viwanda, na kuendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na
fedha za kigeni.
Amesema
uamuzi wa kuongeza usimamizi katika uzalishaji wa mazao hayo makuu ya
biashara unatokana na ukweli kwamba, kwa kipindi kirefu uzalishaji
ulishuka kutokana na changamoto kadhaa.
“Miongoni
mwa changamoto hizo ni kupungua tija katika uzalishaji, baadhi ya
wakulima kuacha kulima mazao hayo kutokana na kukata tamaa kwa sababu
mbalimbali zikiwemo vyama vya ushirika kutotekeleza vema wajibu wao,
wizi, dhuluma na pia ushiriki mdogo wa maafisa kilimo katika kusimamia
kilimo cha kitaalamu,” alisema.
Alizitaja
sababu nyingine za kushuka uzalishaji wa mazao hayo kuwa ni huduma
zisizoridhisha za ugani na utafiti, ukosefu wa pembejeo bora, utitiri wa
tozo na wingi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika.
Akitolea
mfano, Waziri Mkuu alisema uzalishaji wa pamba ulipungua kutoka tani
456,814 mwaka 2013/2014, hadi tani 282,809 mwaka 2015/2016. Kwa upande
wa tumbaku, Waziri Mkuu alisema uzalishaji katika kipindi cha miaka
minne ulishuka kutoka tani 126,624 mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani
60,929 mwaka 2015/2016.
“Serikali
imechukua hatua za kuimarisha utawala bora kwenye vyama vya ushirika
kwa kusimamia chaguzi za vyama 2,537, chaguzi za viongozi wa bodi za
vyama vya ushirika 532 na kufanya kaguzi katika vyama vya ushirika 2,896
vikiwemo vyama vikuu. Kazi za kusimamia vyama vya ushirika
zinaendelea,” alisema.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu alisema Serikali inasimamia uendelezaji wa mazao
hayo moja kwa moja kupitia maafisa kilimo na Bodi za Mazao na kwamba
imechukua hatua za kufuta baadhi ya tozo zilizokuwa kero katika mazao
makuu ya biashara pamoja na kuhakikisha kwamba mauzo yanafanyika kwa
njia ya wazi na inayoleta ushindani.
“Kutokana
na hatua zinazochukuliwa na Serikali kusimamia mazao makuu ya biashara,
tayari tumeanza kuona matokeo chanya kwa kuongezeka uzalishaji wake.
Kwa mfano, hadi mwezi Machi 2018, uzalishaji wa mazao ya asili ya
biashara ulifikia tani 804,025. Uzalishaji huu unaashiria ongezeko la
mavuno ikilinganishwa na mwaka 2016/2017. Ongezeko hilo la uzalishaji wa
mazao ya biashara linakwenda sambamba na kuimarika kwa mwenendo wa bei
za mazao hayo hususan korosho na kahawa,” alisema.
Waziri
Mkuu aliliomba Bunge likubali kupitisha sh. 143,618,762,698 zikiwa ni
makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2018/2019
ambapo sh. 74,527,321,698 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh.
69,091,441,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile,
Waziri Mkuu aliliomba Bunge liidhinishe sh. 125,521,100,000 kwa ajili
ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 117,205,487,000 ni kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na sh. 8,315,613,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO, APRILI 4, 2018
0 comments:
Chapisha Maoni