WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema ukaguzi unaofanywa kwenye bandari ya Dar
es Salaam kwa wasafiri wanaokwenda Zanzibar, hauna lengo la kuwabagua
bali ni kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nchi.
“Hatulengi
kuzuia biashara za wafanyabiashara ndogondogo, bali tunaimarisha
ukaguzi ili kuzuia wasafirishaji wa dawa za kulevya, wasambazaji na
wauzaji,” amesema.
Ametoa
kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Aprili 19, 2018) Bungeni mjini Dodoma
katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati
akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Bw. Jaku Hashim Ayoub
aliyetaka kupata kauli ya Serikali juu ya kuwapunguzia makali
wafanyabiashara wanaotoka Zanzibar.
Waziri
Mkuu amesema: “Wanaofanya ukaguzi pale bandarini siyo watu wa TRA peke
yao kama Mheshimiwa Jaku alivyosema, bali tukumbuke kuwa Tanzania
imeingia katika vita ya dawa za kulevya, kwa hiyo tunaimarisha ulinzi wa
mipaka yetu.”
“Tanzania
inapambana na matumizi ya dawa za kulevya, kwa hiyo ukaguzi huu
umelenga kuzuia watumiaji, wasambazaji na wasafirishaji wa dawa hizo.
Upekuzi huu umelenga kupunguza hili tatizo, umelenga abiria wote na siyo
Wazanzibari peke yao,” amesisitiza.
Amesema
Serikali inaendelea na mipango ya kutafuta mitambo ya kisasa ya kukagua
mizigo ya wasafiri wanaotumia bandari za Tanzania bara.
Mapema,
akiuliza swali lake, Mhe. Jaku alisema: “Kilio cha wabunge wengi
wanaotoka Zanzibar hapa Bungeni ni bandari ya Dar es Salaam kutoza kodi
wafanyabiashara wadogo wanaosafirisha TV au vyerehani. Ni lini utakaa
nao au kufanya ziara ya kushtukiza ili ujionee hali halisi?”
0 comments:
Chapisha Maoni