WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeongeza idadi ya Wakaguzi wa
Mazingira kutoka 62 hadi kufikia 512 ili kuimarisha ukaguzi wa masuala
ya hifadhi ya mazingira nchini.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati
akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa
mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019
kwenye mkutano wa 11 wa Bunge.
Amesema
katika mwaka wa fedha uliopita, jumla ya kaguzi 380 zimefanyika kwenye
viwanda kwa lengo la kufanya tathmini za mazingira pamoja na kutoa elimu
na uelewa kuhusu uendeshaji endelevu wa viwanda unaozingatia utunzaji
bora wa mazingira.
“Kama
nilivyoeleza katika Mkutano wa Kumi wa Bunge hili, halmashauri zote
nchini zinapaswa ziweke mpango mahsusi wa kuhifadhi mazingira
unaojumuisha kupanda na kutunza miti. Serikali itaweka utaratibu wa
upimaji wa utendaji wa wakuu wote wa mikoa na wilaya pamoja na
wakurugenzi wa halmashauri unaozingatia uendelezaji na utunzaji wa
mazingira katika maeneo yao,” alisisitiza.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali inachukua hatua madhubuti za
kuendeleza ardhi kutokana na umuhimu wake kama kitovu cha uzalishaji
mali.
Alizitaja
hatua hizo kuwa ni kutekeleza mpango kabambe wa majiji, manispaa na
miji; kudhibiti migogoro baina ya watumiaji wa ardhi na kuimarisha mfumo
unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi nchini.
“Napenda
kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba Mipango Kabambe ya Manispaa za
Iringa, Singida na Mji wa Kibaha imekamilika na mipango mingine 20 ipo
katika hatua mbalimbali za uandaaji. Hadi sasa, michoro 1,110 ya mipango
miji imeshaidhinishwa kati ya 1,148 iliyopokelewa kutoka Halmashauri za
miji mbalimbali,” alisema.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wote wanapofanya shughuli za
maendeleo, wazingatie mipango kabambe inayoandaliwa na mamlaka za
upangaji miji kwenye maeneo yao husika.
Alisema
Serikali imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na changamoto ya
migogoro ya ardhi miongoni mwa watumiaji ikiwemo migogoro ya mipaka ya
vijiji, wakulima na wafugaji, wanavijiji na hifadhi na mapori ya akiba.
“Moja
ya hatua zilizochukuliwa ni kuunda timu ya kisekta ya kushughulikia
migogoro ya ardhi ambayo imetembelea mikoa ya Geita, Kagera, Katavi,
Morogoro na Tabora na kufanya majadiliano na wadau 1,106. Hatua
mbalimbali za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinaendelea kuchukuliwa.”
Kuhusu
utendaji wa bandari nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea
kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kuifanya Tanzania iwe kitovu cha
usafiri wa majini. Alisema uboreshaji huo utaanza na gati namba moja
hadi saba; kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia meli na eneo la
kugeuzia meli; kuimarisha mtandao wa reli bandarini pamoja na kujenga
gati maalumu la kuhudumia meli za magari.
“Vilevile,
Mamlaka ya Bandari Tanzania imefungua ofisi katika baadhi ya nchi
jirani kwa lengo la kuongeza urahisi wa kutoa huduma. Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaendelea na uboreshaji wa bandari za Dar es
Salaam, Tanga na Mtwara,” alisema.
“Serikali
itatekeleza mradi wa dirisha moja la forodha (Tanzania Electronic
Single Window System-eSWS) ili kuwaweka pamoja wadau wote wa kuondosha
shehena bandarini na mipakani. Kukamilika kwa mradi huo, kutarahisisha
na kupunguza muda na gharama za utoaji na upitishaji wa shehena
bandarini,” alisema Waziri Mkuu.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa awamu ya tatu ya
mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umejumuisha ujenzi wa mtandao wa
miundombinu ya itifaki (Internet Protocol – Multiplier Label Switching)
pamoja na ujenzi wa kituo cha kuhifadhi data ambacho hadi sasa mifumo
ya taasisi 27 imeunganishwa ukiwemo mfumo wa ukusanyaji mapato wa TRA.
“Kukamilika
kwa ujenzi wa kituo hicho kutaongeza usalama, usiri wa data, kujikinga
na majanga na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali na muingiliano wa
mifumo katika Kituo cha Data cha Taifa na vituo vingine vitakavyojengwa
nchini,” alisema.
Kuhusu
huduma ya mawasiliano vijijini, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea
na ujenzi wa miundombinu ambapo vijiji 1,921 vimepatiwa huduma hiyo.
“Serikali imeimarisha huduma za simu na intaneti katika taasisi za umma
zikiwemo shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na ofisi za posta.
“Katika
mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kujenga Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano na kupanua matumizi yake hadi katika ngazi ya wilaya na
kuzisimamia kampuni za simu nchini ili ziweze kutoa kumbukumbu sahihi
kwa lengo la kukokotoa mapato yatokanayo na malipo ya huduma za simu za
kitaifa na kimataifa,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO, APRILI 4, 2018
0 comments:
Chapisha Maoni