MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyelazwa nchini Ubelgiji anatarajiwa kurudi nyumbani siku yoyote kuanzia juzi, baada ya madaktari kumaliza kumpatia matibabu, amesema.
Lissu ambaye amekuwa hospitalini tangu Septemba 7, mwaka jana aliposhambuliwa nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma, aliliambia shirika la utangazaji la BBC juzi, kuwa kwa sasa hana tena kidonda cha risasi na yupo tayari kurudi nyumbani.
"Sina tena kidonda cha risasi, nilipigwa mara 16," alidai Lissu (50) na kufafanua "sina tena kiungo kilichovunjwa". "Nilikuwa nimevunjwa mguu mmoja mara tatu, mikono yote ilikuwa imevunjwa, nilikuwa na risasi nyingi mwilini, na vidonda vingi."
Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema viungo vyote vilivyokuwa vimevunjika vimeshaunga. Alisema tangu aanze kupata matibabu amefanyiwa operesheni 17, nne zikiwa sehemu ya tumbo, lakini sasa hali yake ni nzuri.
Lissu alisema analazimika kurundi nchini kwa kuwa yeye ni Mbunge, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri kivuli wa Sheria na Katiba. Alisema kwa majukumu hayo hawezi kwenda mafichoni. "Siwezi kwenda mafichoni, siwezi kuikimbia nchi yangu, nitarudi Tanzania," alisema. "Mimi ni mbunge, mimi ni kiongozi bungeni, ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, mimi ni msemaji wa sheria na katiba wa chama changu."
Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana kaka wa Lissu, wakili Alute Mughwai alisema familia bado haijapokea taarifa ya siku anayotarajia kurudi. Alisema familia inachofahamu ni kuwa Lissu amefanyiwa operesheni ya 19 wiki chache zilizopita, hivyo kutakuwa na uangalizi wa afya yake.
“Hayo mahojiano aliyofanya juzi sijayaona, nitawasiliana naye leo jioni (jana) nimsikilize, lakini sisi kama familia hatujapata taarifa yoyote lini atarudi, wala hatuwezi kujua hadi tupewe taarifa na hospitali,” alisema wakili Mughwai.
Lissu alipoulizwa na BBC endapo amepata msaada wa matibabu kutoka serikalini, alisema chombo pekee chenye wajibu wa kumgharamia matibabu yake ni Bunge na "siyo serikali, wala Ikulu, wala mtu yoyote."
0 comments:
Chapisha Maoni