Spika
wa Bunge, Job Ndugai amesema utaratibu wa Bunge kugharamia matibabu ya
Tundu Lissu unaendelea kufanyiwa kazi na ukikamilika utatolewa
ufafanuzi.
Spika
Ndugai ametoa kauli hiyo jana Alhamisi Aprili 5, 2018 wakati akihojiwa
na Kituo cha Televisheni cha Azam ikiwa ni siku moja kupita tangu
aliporejea nchini akitokea India kwa matibabu.
Lissu
ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema
alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7, 2017 na kupelekwa
Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya
Nairobi ambako alilazwa hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji katika
Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, anakoendelea na matibabu.
Tangu
wakati huo, familia yake na viongozi wa Chadema wamekuwa
wakililalamikia Bunge kutogharamia matibabu ya mbunge huyo huku Lissu
naye mara kadhaa akizungumzia jambo hilo.
Lakini
katika mahojiano hayo aliyofanya na mtangazaji wa televisheni hiyo,
Charles Hilary, Ndugai amesema, “Lile tukio (la kushambuliwa Lissu)
limekuwa ni jipya, linataka watu wengi waweze kuangalia jinsi ya
kufanya. Kwa kifupi kila anayekwenda kutibiwa nje anakuwa na barua ya
Wizara ya Afya au kibali kutoka Muhimbili, ndivyo sisi Watanzania
tunafanya.”
“Hiyo
ni kwa mbunge na asiye mbunge, hata mwananchi wa kawaida utaratibu ndio
huo. Sasa kwa mheshimiwa Lissu alivyotoka Dodoma kila mtu anafahamu
alipewa rufaa Nairobi na ndio maana tunaona kwa wabunge wengine wote
wanaotibiwa kwa utaratibu huu huwa hawachangiwi hata na Bunge lenyewe.”
Amefafanua
zaidi kuwa, “lakini mheshimiwa Lissu pale pale tulichanga sisi wenyewe
wabunge kama wabunge kwa sababu tulikuwa tunajua safari hii ina tatizo
ndio maana ikabidi watu wachange kutoka mfukoni.”
Amesema
ni sawa na mtu aliyekata rufaa yeye mwenyewe kwenda katika hospitali
aliyochagua, “kwa maana ile hakuchagua yeye mheshimiwa Lissu lakini
familia yake na chama chake na kadhalika, halijawahi kutokea jambo kama
lile katika Bunge letu, lina upya wa aina yake.”
Amesema upya huo unahitaji ushirikiano mkubwa wa familia na Bunge kuweka utaratibu ambao hautakuwa kwa kwa Lissu pekee.
“Hata
kesho na keshokutwa huo ndio utakuwa utaratibu utatumika siku zijazo,
kwa hiyo bado linafanyiwa kazi siku ya siku litakuja kutolewa maelezo
kama linawezekana au haliwezekani.”
Kuhusu wabunge kupewa ulinzi baada ya Lissu kushambuliwa, Spika Ndugai amesema Dodoma hali ya ulinzi ni kubwa.
“Dodoma
ni salama na tumemwomba RPC wakati wa Bunge na wakati wote ulinzi uwepo
na umeimarishwa na sidhani kama litatokea tena,” amesema.
0 comments:
Chapisha Maoni