SERIKALI
imesema hakuna haja ya kubadilisha sheria ya uzazi iliyopo kwa sasa,
sababu inampa fursa mwanamke kupumzika kutozaa mara kwa mara na kufuata
uzazi wa mpango kama nchi inavyoelekeza na si vinginevyo.
Hayo
yamesemwa Bungeni leo, Aprili 18 mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George
Mkuchika, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Sonia Juma
Magogo, aliyetaka kufahamu mpango wa serikali wa kutaka kuwasaidia kina
mama ambao wanajifungua kabla ya kipindi cha kuruhusiwa kupata miezi
mitatu ya mapumziko ili waweze kuwanyonyesha vichanga na kuendelea
majuKumu yao ya kazi.
“Kwa
mujibu wa kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2009, mtumishi wa umma
anapojifungua hupewa likizo ya malipo ya siku 84, endapo atajifungua
zaidi ya mtoto mmoja (mapacha) ataongezewa siku 14 na kuwa jumla ya siku
98.
“Lakini
mtumishi akijifungua mtoto tena kabla ya kutimiza miaka mitatu, atapewa
likizo maalum ya wiki sita ili kuhudumia mtoto wake kwa mujibu wa
kanuni na baada ya hapo serikali inaweza kumuongezea siku za kupumzika
kulingana na ushauri wa daktari.
“Ikumbukwe
kwamba, likizo ya uzazi hutolewa mara moja katika kipindi cha miaka
mitatu kwa kuzingatia sera ya afya ya mama na mtoto inayosisitiza
kulinda na kujenga afya ya mama na mtoto na kuhimiza uzazi wa mpango.
Sheria hizi ni za nchi nzima hivyo zinapaswa ziheshimiwe na kufuatwa kwa
watumishi wa serikali na mashirika ya umma.
Aidha,
Mbunge Mgila alisema uzazi wa mpango ni makubaliano ya wanandoa ikiwemo
lini wazae na kuitaka serikali kubadilisha sheria hiyo ya likizo ambapo
Waziri Mkuchika amesema kuzaa baada miaka mitatu inatosha huku akisema
wanaume wawahurumie wanawake wanaowazalisha kila mwaka kwani nao
wanahitaji kupumzika.
Mkuchika
ametoa rai kwa watumishi wa umma au sekta binafsi, kuwa endapo yeyote
atanyimwa haki ya likizo ya uzazi aitaarifu wizara husika ili hatua
stahiki zichukuliwe dhidi ya mwajiri wake.
0 comments:
Chapisha Maoni