Serikali
imesema kuwa haitasitisha mkataba na Mwekezaji wa Kampuni ya Chai
Maruku, iliyoko mkoani Kagera, kwa sababu mgogoro wa malipo uliopo baina
ya kampuni hiyo na wakulima pamoja na wafanyakazi wake unaelekea
kutatuliwa.
Hayo
yameelezwa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi
la Mbunge wa Bukoba Vijijini Mhe. Jason Rweikiza (CCM), aliyetaka kujua
sababu za Serikali kutovunja mkataba na mwekezaji huyo na kurejesha
umiliki kwa Serikali au kwa mwekezaji mwingine atakayejali maslahi ya
wakulima na wafanyakazi.
Katika
swali lake la msingi, Mhe. Rweikiza alisema kuwa tangu Kampuni hiyo
ibinafsishwe kwa mwekezaji, kumekuwa na malalamiko ya wakulima
kutolipwa fedha za mauzo ya chai kwa wakati na wafanyakazi kutolipwa
mishahara na stahiki zao ipasavyo.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa, katika kutatua mgogoro huo Serikali kupitia ofisi
ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa utendaji
na uendeshaji wa Kampuni hiyo kwa kufanya vikao kwa nyakati tofauti kwa
kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kagera, Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chai
(TASHTIDA).
Alisema
kuwa katika vikao hivyo haki ya kila upande ilizingatiwa ikiwemo suala
la haki za wafanyakazi pamoja na madai ya wakulima, ambapo mpaka sasa
mwekezaji amekubali kulipa madai ya wakulima kiasi cha Sh. milioni 12
huku wakiendelea kujadili namna ya kutatua suala la madai ya
wafanyakazi.
Dkt.
Kijaji aliahidi kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala
hilo ili kuhakikisha haki za wakulima na wafanyakazi hazipotei.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
4/4/2018
0 comments:
Chapisha Maoni