Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amezishauri kampuni zinazotengeneza vilevi kutengeneza pombe yenye ladha ya gongo, kwa kuwa baadhi ya wateja wanavutiwa na ladha hiyo wana wanakipenda kinywaji hicho.
Mwijage
ameyasema hayo leo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Viti Maalumu, Gimbi Masaba (Chadema) aliyehoji mpango wa
serikali wa kuanzisha na kuhalalisha viwanda vya kutengeneza pombe aina
ya gongo ili kuchochea uchumi wa nchi na kubainisha kuwa, gongo
ikitengenezwa kiwandani itafuata ubora unaotakiwa kisheria.
“Moja
ya kigezo muhimu cha kuanzisha kiwanda ni uwepo wa soko, kutokana na
wananchi kupenda kinywaji hiki(gongo) nawashauri wadau wa sekta hii
kuwasiliana na ofisi za Sido ambazo zinapatikana mikoa yote ili kupata
muongozo juu ya uanzishaji wa viwanda bora na salama vya aina hii,” alisema Mwijage.
Amesema
haiwezekani Serikali kuhalalisha gongo, ila inaishauri sekta binafsi
kuanzisha viwanda vitakavyotumia malighafi zinazotengeneza kinywaji
hicho kwa lengo la kuzalisha kinywaji kinachokidhi viwango vya usalama
na ubora wa chakula.
Katika swali la nyongeza, Masaba amehoji kama serikali ipo tayari kufanya utafiti kujua faida zilizo kwenye gongo.
Mwijage
amesema faida zinafahamika, lakini atawaelekeza wataalamu wake waendele
maeneo yenye gongo na pombe nyingine za kienyeji ili kuzifanyia utafiti
na zitengenezwe kwa kufuata ubora na viwango.