Kamati
ya Bunge ya Katiba na Sheria imesema katika bajeti ya Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) mwaka 2017/18 kuna ongezeko la fedha
lililotokana na gharama za kuhamisha watumishi wa ofisi hiyo kutoka Dar
es Salaam kwenda Dodoma, kwamba ongezeko hilo ni zaidi ya fedha
zilizoidhinishwa na Bunge.
Akisoma
taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa bajeti ya ofisi hiyo kwa
niaba ya mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, mbunge wa Viti
Maalum (CCM), Amina Mollel amesema katika mwaka wa fedha 2017/18 ofisi
binafsi ya makamu wa rais ilitengewa Sh4.9bilioni kwa ajili ya matumizi
ya kawaida.
Amesema
hadi kufikia Februari 2018, ofisi hiyo ilipokea Sh5bilioni sawa na
asilimia 103 ya bajeti ya matumizi ya kawaida, ikiwa ni ongezeko la
asilimia tatu.
“Kiasi
hicho kiliongezeka kutokana na gharama za kuhamisha watumishi wa ofisi
ya makamu wa Rais kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma,” amesema.
Amebainisha
kuwa pia ofisi hiyo mwaka 2017/18 ilitengewa Sh8.2bilioni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida, kwamba hadi kufikia Machi 2018 ofisi hiyo ilipokea
Sh10.5bilioni sawa na asilimia 128 ya bajeti ya matumizi ya kawaida,
ikiwa ni ongezeko la asilimia 28 zaidi ya fedha zilizoidhinishwa na
Bunge.
“Uchambuzi
huu unaonyesha kumekuwa na mwenendo mzuri na wa kuridhisha kuhusu
upatikanaji wa fedha kwa ofisi ya makamu wa rais. Maoni ya kamati ni
kwamba hali hii ya upatikanaji wa fedha kwa wakati inatakiwa kuendelea
na kuzingatiwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19,” amesema Mollel.


0 comments:
Chapisha Maoni