Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
tarehe 07 Aprili, 2018 ameungana na Watanzania wote kuadhimisha siku ya
mmoja wa waasisi wa Taifa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa
Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi kwa
kuzindua kituo cha polisi, kufungua nyumba 31 za askari polisi na
kushuhudia maonesho ya Polisi katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri
Abeid Jijini la Arusha.
Kituo
cha polisi cha watalii na wanadiplomasia kilichopo Naura, kituo cha
polisi cha Muriet, na nyumba za 18 kati ya 31 za makazi ya polisi
vimejengwa kwa mchango wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha na Benki ya
CRDB kwa gharama ya Shilingi Milioni 753, wakati nyumba za polisi 13
zimejengwa na Serikali kwa gharama ya Shilingi Milioni 250.
Mhe.
Rais Magufuli aliagiza kujengwa kwa nyumba hizo baada ya kutokea ajali
ya moto iliyosababisha nyumba 13 za makazi ya askari polisi na mali zao
kuungua moto tarehe 27 Septemba, 2017.
Katika
kutekeleza agiza hilo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo akaamua
kuwashirikisha wafanyabiashara na benki ya CRDB kuchangia ujenzi huo na
kufanikiwa kujenga nyumba nyingine 18 na vituo hivyo viwili vya polisi.
Pamoja
na kuzindua miradi hiyo Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia maonesho ya
Jeshi la Polisi ya kuzuia na kupambana na uhalifu yakiwemo kukabiliana
na waandamanaji haramu, wezi, waporaji watumiao silaha na magaidi,
yaliyofanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.
Akizungumza
baada ya maonesho hayo Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa litaendelea
kumkumbuka Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kwa juhudi zake za kujenga
nchi ikiwemo kuwajengea makazi wananchi masikini kule Zanzibar na ametoa
wito kwa Watanzania kumuenzi kwa kudumisha amani na kuchapa kazi.
Pamoja
na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo kwa jitihada zake
za kuwaunganisha wadau na kisha kufanikiwa kujenga nyumba za askari na
vituo vya polisi Mhe. Rais Magufuli ametoa Shilingi Bilioni 10
kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari polisi wa vyeo vya chini
nchini, na amewaagiza viongozi wa mikoa yote kuwashirikisha wadau katika
ujenzi huo kama ilivyofanyika mkoani Arusha ili kukabiliana na tatizo
la askari kukosa nyumba za makazi.
“Askari
polisi mnafanya kazi kubwa sana ya kulinda raia na mali zao, natambua
juhudi kubwa mnazofanya na napenda kuwashukuru sana, naomba Watanzania
wote tuendelee kuliunga mkono Jeshi la Polisi.
“Wakati
naingia madarakani kulikuwa na mauaji kila wakati, kule Kibiti pekee
yake waliuawa watu 59 wakiwemo askari polisi 17 na raia 42, Jeshi la
Polisi limefanya kazi kubwa na sasa mauaji yale yamedhibitiwa, ni lazima
tulipongeze jeshi letu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amekubali maombi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP
Simon Sirro la kuongezewa idadi ya askari na kupandishwa vyeo kwa
maafisa wa polisi ambapo ameruhusu Jeshi la Polisi kuajiri askari wapya 1,500 kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kumpelekea mapendekezo ya maafisa wanaostahili kupandishwa vyeo.
Mhe.
Rais Magufuli amempongeza IGP Sirro kwa hatua ya kuwafukuza kazi askari
polisi 458 waliokutwa na makosa ya kinidhamu na uadilifu kuanzia mwaka
2015 hadi sasa, na ametaka hatua hizo ziendelee kuchukuliwa dhidi ya
askari wengine wanaokiuka maadili na taratibu za kazi ili kuondoa
malalamiko kutoka kwa wananchi yakiwemo upokeaji rushwa na unyanyasaji
raia kwa kuwabambikiza kesi.
Halikadhalika
Mhe. Rais Magufuli amepiga marufuku askari, maafisa wa polisi na
viongozi wengine wa Serikali kushiriki ufyekaji wa mashamba ya bangi na
badala yake ametaka mashamba hayo yanapobainika yafyekwe na wanavijiji
wenyewe waliohusika kuyalima.
Maadhimisho
hayo yamehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli na viongozi
mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, viongozi wakuu wa vyombo
vya ulinzi na usalama, wabunge na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Arusha
07 Aprili, 2018


0 comments:
Chapisha Maoni