Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amefungua barabara ya lami ya Iringa – Migoli – Fufu yenye urefu wa
kilometa 189 na ambayo inaunganisha Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Dodoma.
Barabara
hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town nchini
Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri (The Great North Road) imejengwa
kwa gharama ya Shilingi Bilioni 207.457 ikiwa ni ufadhili wa benki ya
maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Japan (JICA) kwa asilimia 21.3 na Serikali ya Tanzania
imetoa asilimia 12.8.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale
amesema kukamilika kwa barabara hiyo kumeondoa adha iliyowakumba
wananchi kwa miaka mingi ambapo safari ya Iringa – Dodoma iliyochukua
siku nzima ama siku kadhaa wakati wa mvua, sasa inachukua muda wa saa
2:30.
Balozi
wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida na Mwakilishi wa AfDB Bw.
Jeremy Aguma wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa
miradi inayofadhiliwa na taasisi zao, na wameahidi kukuza zaidi
ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayosaidia
kukuza uchumi wa wananchi kama inavyoelekezwa katika dira ya maendeleo
ya mwaka 2025.
Wabunge
wa Mkoa wa Iringa wakiongozwa na Mbunge wa Ismani na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi
wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake zilizoyawezesha majimbo
yao kupata miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, vituo vya afya
na zahanati, Maji, uwanja wa ndege wa Nduli, Umeme, ruzuku ya elimu na
dawa.
Akizungumza
na wananchi waliojitokeza katika ufunguzi wa barabara hiyo Mhe. Rais
Magufuli amewapongeza kwa kupata barabara ya uhakika na amewataka
kuongeza juhudi katika uzalishaji mali hasa katika kilimo na biashara
ili waweze kunufaika nayo.
Mhe.
Rais Magufuli amezishukuru AfDB na JICA kwa kuendelea kuwa washirika
muhimu wa maendeleo ya Tanzania, na kwa namna ya pekee amempongeza
Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale kwa uchapakazi wake,
ubunifu, uaminifu na uadilifu uliomwezesha kuiongoza TANROADS kwa
mafanikio hasa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa
barabara na madaraja.
Mhe.
Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga barabara hiyo, Serikali
inauboresha uwanja wa ndege wa Nduli ili uweze kupokea ndege kubwa
zitakazoleta watalii wengi na wafanyabiashara katika mkoa wa Iringa na
maeneo mengine ya kusini mwa Tanzania ili rasilimali zilizopo katika
maeneo hayo ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ziwanufaishe wananchi kama
wanavyonufaika wananchi wa Kaskazini mwa Tanzania.
“Ruaha
ni hifadhi kubwa, nataka hifadhi hii iwe kitovu cha utalii, nataka
nyinyi ndugu zangu wa Iringa mnufaike na utalii katika hifadhi hii kama
wanavyonufaika kule kaskazini kupitia Serengeti, watalii wakija hapa
wenye hoteli watapata wateja, wenye maziwa watauza, wenye matunda
watauza, wenye mahindi watauza, mtapata hela” amesema Mhe. Rais
Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Iringa kuwapuuza wanaodai
Serikali inakopa sana, na kueleza kuwa fedha hizo hukopwa kwa masharti
nafuu, riba ndogo na hulipwa kwa muda mrefu, na kwamba ndizo zinatumika
kujenga miundombinu ya kuchochea uchumi.
Pamoja
na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli sherehe hizo pia zimehudhuriwa
na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino
Ndugai, Mawaziri, Wabunge kutoka kamati ya bajeti na kamati ya
miundombinu, Maaskofu na viongozi wa vyama vya siasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Iringa
0 comments:
Chapisha Maoni