Na: Frank Shija – MAELEZO, Mbeya.
Serikali
inaendelea na mikakati wa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma
bora za afya na kwa wakati ili kuleta ustawi katika kufikia azma ya
Tanzania ya viwanda.
Hayo
yamebainishwa jana Jijini Mbeya na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa
Mbeya, Constantine Mushi alipokuwa akizinduzi mafunzo kwa wakufunzi wa
kitaifa kuhusu Bima ya Afya ya Jamii (CHF), mfumo wa kupeleka fedha moja
kwa moja katika vituo vya kutolea huduma (DHFF), na mfumo wa manunuzi
ya dawa nje ya mfumo wa kawaida wa MSD (Jazia – Prime Vendor System).
Kaimu
Katibu Tawala huyo aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuhakikisha wananchi wake
wanakuwa na afya ya uhakika kwa kupata huduma bora za afya na kwa
wakati, jambo lililopelekea kuanzishwa kwa utaratibu wa kupeleka fedha
moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma tofauti na ilivyokuwa hapo
nyuma.
“lengo
mahususi ya mafunzo haya ni kuelewa kwa upana maana ya ugatuaji wa
mipango ya afya na bajeti kwa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja
kwenye vituo vya kutolea huduma (DHFF)”yenye matarajio ya kupunguza
urasimu na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kuimarisha
uwajibikaji na uboreshaji wa uandaaji wa mipango, bajeti na matumizi
yanayolenga kuboresha huduma za afya,” alisisitiza.
Aliongeza
kuwa mpaka sasa katika robo ya pili ya mwaka Serikali imekwisha peleka
takribani shilingi bilioni 45 katia jumla ya vituo vya kutolea huduma za
afya 5,125 nchi nzima.
Aidha
Mushi alibainisha kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa afya kwa
wananchi imekuwa na mikakati ambayo inashirikiana na wadau wa maendeleo
katika kuitekeleza ikiwemo utekelezaji wa maboresho ya mifumo ya sekta
za umma inayoratibiwa na TAMISEMI kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa
Marekani kupitia Shirika lake la maendeleo USAID/PS3 ambao unatekelezwa
katika mikoa 13 ya Tanzania Bara.
“Napenda
kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo ambao
tumeendelea kushirikiana nao katika Nyanja mbalimbali, kwa kipekee
niwashukuru wenzetu wa Wadau wa Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket
Fund), HPSS, PS3, Global Supply Chain Program, Boresha Afya – Deloitte,
World Vision. EGPAF, Jhpiego, GIZ, AGPAHI na Pharmaccess,” aliongeza.
Akitoa
muongozo wa mafunzo hayo Mwakilishi kutoka OR- TAMISEM, Bi. Nkinda
Shekalage alisema kuwa mafunzo haya yataleta chachu katika kufikia
malengo ya utoaji wa huduma za afya zilizo bora na kwa ufanisi endapo
washiriki wataenda kutekeleza wajibu wao wa kuwafundishi waliochini yao
kama ilivyokusudiwa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Fedha wa PS3, Dkt. Gemini Mtei
alisema kuwa PS3 imeshirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuiunda DHFF
kwa ajili ya kuwezesha vituo vya kutolea huduma za afya kupokea fedha za
Mfuko wa Afya wa Pamoja(HBF) moja kwa moja kwenye akaunti zao.
Dkt.
Gemini alisema kuwa msaada uliotolewa na PS3 ni wa kitaalam, ili
kuwezesha kuwepo kwa mfumo mzuri wa upokeaji wa hizi fedha. Sambamba na
hilo, PS3 imeshirikiana na Serikali kuweka mifumo itakayowezesha DHFF
kufanikiwa, mifumo hii ni Mfumo wa Uhasibu na Utoaji Taarifa kwenye
Vituo vya Kutolea Huduma (FFARS) pamoja na Mfumo wa Mipango, Bajeti na
Utoaji wa Taarifa (PlanRep).
“Niseme
tu kuwa DHFF haiwezi kufanya kazi vizuri endapo hakuna mifumo thabiti
ya mipango na bajeti katika ngazi ya kutolea huduma, ndio maana PS3
imesaidia katika hilo, na mifumo hiyo miwili (PlanRep na FFARS)
ilizinduliwa mwezi Septemba 2017 na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa”.
Alifafanua Dkt. Gemini.
Aliongeza
PS3 itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza uimarishwaji
wa mifumo mbalimbali inayolenga kuboresha sekta ya afya na sekta
nyinginezo, kulingana na mahitaji ya Serikali.
Mradi
wa PS3 umesaidia pia kujenga uwezo kwa Serikali katika maeneo ya
utekelezwaji wa mpango wa DHFF, CHF iliyoboreshwa, na PV. USAID kupitia
PS3 imewezesha mafunzo ya wakufunzi wa kitaifa yaliyofanyika mjini
Morogoro wiki moja iliyopita, na pia ndiyo inayofadhili mafunzo
yaliyoanza leo katika mikoa minne: Mbeya, Mwanza, Morogoro na Mtwara.
Mafunzo haya yamehusisha maafisa kutoka mikoa yote iliyo Tanzania bara,
na baadaye yatashuka kwenda ngazi ya Halmashauri na kwingineko.
Mafunzo
haya yamekuja kufuatia kuanza kwa kubainika kwa changamoto katika
utekelezaji wa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo
vya kutolea huduma za afya (Direct Health Facility Financing) ili kuzipa
nguvu zaidi Kamati za Usimamizi wa Huduma za Afya (HFGC) katika kupanga
na kusimamia huduma za Afya katika ngazi ya jamii uamuzi uliotokana na
mkutano wa mwaka wa mapitio ya Sekta ya Afya (Joint Annual Health Sector
Review) uliofanyika Desemba 7, 2016.
0 comments:
Chapisha Maoni