Mtoto wa miezi sita, Halfani Lema, mkazi wa Mtaa wa Ibanda Kata ya Nyegezi amefariki dunia saa chache baada ya mama yake kuachiwa kutoka Kituo cha Polisi Igogo, Nyegezi jambo ambalo limeibua utata.
Mama wa mtoto huyo, Ashura Theonest (26) alikamatwa na
polisi Aprili 2, akidaiwa kuiba simu ya jirani yake hivyo kupelekwa
mahabusu akiwa na mtoto wake.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Vedastus Mushola alisema jana
kwamba mama huyo alipofikishwa kituoni hapo aliwaomba askari waliokuwa
zamu ajidhamini ili arudi nyumbani kwani hakuwa na maziwa ya
kumnyonyesha mwanaye usiku kucha lakini hakuruhusiwa.
“Pamoja na mwanamke huyo kueleza sababu hiyo, hakuna askari
aliyemruhusu, lakini baadaye usiku hali ya mtoto ilibadilika na Aprili 3
mchana ndipo walimruhusu kwenda hospitali ya Wilaya Butimba kwa ajili
ya matibabu,” alidai Mushola.
Mwenyekiti huyo alisema mtoto huyo alifariki dunia baada ya
kufikishwa hospitali wakati akitibiwa jambo lililozua hasira kwa wakazi
wa eneo hilo wakisema polisi ndiyo waliosababisha kifo hicho.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
alisema si kweli kwamba polisi ndio waliosababisha kifo cha mtoto huyo
akisema mama wa mtoto alijidhamini na kuruhusiwa kwenda nyumbani, “Yule
mama alipofika nyumbani mtoto wake, aliumwa akampeleka hospitalini na
alifia hospitali. Hizi taarifa za kwamba mtoto alifia kituoni si za
kweli, kwanza kituo cha Igogo hakina mahabusu ya wanawake kuna mahabusu
ya wanaume tu, kwa hiyo ukweli ndio huo.”
Mushola alilitaka jeshi la polisi kuwashirikisha wenyeviti
wa mitaa husika pindi yanapotokea matukio kwenye mitaa yao ili kuepusha
adha kama hizo, “Matukio madogomadogo yawe yanasuluhishwa kwenye uongozi
wa mtaa, kwanza mimi nilikuwa sijui tukio hilo hatujashirikishwa mpaka
linafika polisi.”
Ashura hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa sasa akieleza
kuwa ana maumivu makali ya kupoteza mtoto wake lakini wananchi wenzake
wa Mtaa wa Ibanda walisusia msiba huo wakitaka maelezo ya kina kutoka
polisi.
Hali hiyo ililazimu maiti kukaa mochwari kwa siku tatu hadi
pale uongozi wa polisi ulipotolea ufafanuzi suala hilo ndipo wananchi
walipokubali kumzika mtoto huyo jana katika makaburi ya mtaa huo.
Ofisa utumishi wa Hospitali ya Nyamagana Andrew Chinduo
alisema hakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo lakini alitaka atafutwe
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba
kwani ndiye msemaji mkuu.
Hata hivyo, Kibamba alipotafutwa simu yake iliita bila kupokewa.


0 comments:
Chapisha Maoni