Mkurugenzi
mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao ametangaza kuachia mikoba ya kuiongoza
kampuni hiyo baada ya mkataba wake kufika tamani.
Kutokana
na hilo, Ferrao atakabidhi majukumu kwa mrithi wake, Sylvia Mulinge
kuanzia Juni Mosi na kuhitimisha miaka mitatu ya kuiongoza kampuni hiyo
inayoongoza kwa idadi kubwa ya wateja nchini.
Taarifa
iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya Vodacom, Ali Mufuruki inaeleza
makabidhiano ya ofisi kati ya Ferrao na Sylivia yatafantika kwa miezi
mitatu na kukamilika Agosti 31.
Mufuruki
alimpongeza Ferrao kwa mchango mkubwa alioutoa katika kipindi
alichoiongoza kampuni hiyo pekee iliyofanikiwa kujiorodhesha Soko la
Hisa Dar es Salaam (DSE) licha ya Serikali kuzitaka kampuni zote za
mawasilinao kufanya hivyo.
Nafasi
ya Ferrao itachukuliwa na anayetokea kampuni ya Safaricom ya Kenya
ambako kwa sasa anafanya kazi kama mkurugenzi wa Huduma kwa wateja
aliyojiunga nayo tangu mwaka 2006.
Akizungumzia
kuondoka kwa Ferao jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya
Vodacom, Ali Mufuruki alimpongeza kwa kuiendesha kampuni hiyo kwa
mafanikio tangu alipojiunga nayo mwaka 2015.
“Bodi
inamshukuru Ian kwa uongozi wake makini. Ameivusha kampuni katika
hatua muhimu, akiiacha na jina kubwa Tanzania. Ian ni rasilimali muhimu
kwa Vodacom. Miaka yake mitatu ilikuwa endelevu iliyojaa mikakati na
maoni yaliyoibadilisha Vodacom kufanya biashara kisasa. Anaiacha timu
madhubuti iliyojizatiti kuleta mafanikio,” alisema Mufuruki.
Kabla ya kujiunga na Vodacom Tanzania, Ferrao alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Vodacom nchini Lesotho.
“Ilikuwa
ni nafasi adhimu kuiongoza Vodacom Tanzania katika kipindi cha
mabadiliko na ukuaji. Najisikia fahari kufanya kazi Tanzania na kusaidia
kuipeleka katika ulimwengu wa kidigiti na mabadiliko ya teknolojia,”
alisema.
Sylvia,
aliyekuwa mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa kampuni kubwa zaidi ya
mawasiliano nchini Kenya, Safaricom aliyojiunga nayo tangu mwaka 2006.
Kwa majukumu haya mapya, Sylvia atalazimika kuendeleza mafanikio aliyoyapata Ferrao kwenye ukurugenzi wake.
Licha
ya kufanikiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake DSE zenye thamani ya
Sh476 bilioni na kuwavuta zaidi ya wawekezaji 40,000 wa ndani, tayari
kampuni hiyo imelipa gawio la Sh28.5 bilioni.
“Sera
ya gawio inataka walau asilimia 50 ya faida iliyopatikana itolewe kwa
wanahisa lakini Vodacom imelipa asilimia 60,” inasema taarifa hiyo.
Mwenyekiti
wa bodi alimtakia kila la heri Ferrao na kumkaribisha mkurugenzi mpya
atakayeiongoza Vodacom kuwahudumia Watanzania kwa kuanzia Juni Mosi.
“Tunamtakia
heri Ferrao na familia yake maisha mema. Naomba kumkaribisha mtendaji
mkuu mpya ambaye nina uhakika atafanya kazi na timu ya Vodacom na
tutafurahia mafanikio siku zijazo,” alisema Mufuruki.
0 comments:
Chapisha Maoni