Kifo
cha kutatanisha cha kijana anayejishughulisha na uuzaji wa machungwa
jijini Mbeya, kimeibua vurugu kubwa za vijana wenzake kutokana na
kuhusishwa na Jeshi la Polisi.
Kijana
huyo aliyefahamika kwa jina la Allen Mapunda (20), alifariki dunia,
siku moja baada ya kukamatwa na kukaa mahabusu kisha kupelekwa
hospitali.
Alifia hospitali alikopelekwa kupatiwa matibabu ya majereha baada ya kukamatwa kwa tuhuma za uhalifu ambazo hazijawekwa wazi.
Mapunda alifariki dunia katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya, baada ya kukaa kituo cha polisi kwa siku moja.
Inadaiwa
kuwa kijana huyo mkazi wa Mtaa wa Iyela II anayefanya shughuli zake za
ujasiriamali katika Soko la Sido jijini Mbeya, kabla ya mauti kumkuta
alikamatwa Machi 24, mwaka huu majira ya saa nne usiku katika eneo la
kucheza ‘pool’ Mtaa wa Maendeleo na kumpeleka hadi Kituo Kikuu cha
Polisi.
Inadaiwa
Mapunda alikuwa na vijana wenzake wakicheza mchezo huo na baada ya
kuwaona polisi aliwaambia wenzake wakimbie, lakini wote walitiwa
mbaroni.
Habari
zaidi zinaeleza kuwa Mapunda alikaa kwa siku moja na kesho yake
alidhaminiwa na ndugu ambao waliamua kumpeleka hospitali kwa ajili ya
matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata.
Kwa
mujibu wa mama yake mlezi, Alice Mapunda, marehemu alionekana na
majeraha mkononi na kichwani ambako alikuwa akivuja damu huku
akilalamikia maumivu.
Baada
ya hali ya marehemu kuwa mbaya katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa,
walimpa rufani ambapo alihamishiwa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya
ambapo, alifariki dunia muda mfupi wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Kufuatia
kifo cha kijana huyo, baadhi ya vijana wa Iyela waliamua kuandamana
kupinga tukio hilo, wakidai kuwa linahusishwa na polisi, hivyo walianza
kuwatafuta polisi wanaoishi eneo la kata hiyo na viongozi wa mtaa kwa
nia ya kulipa kisasi.
Miongoni
mwa viongozi waliokumbwa na kadhia hiyo ni Mwenyekiti wa Iyela II, Boaz
Kyejo, ambaye alivunjiwa dirisha la nyumba yake wakimtuhumu kuhusika
kuwaita polisi kwa ajili ya kufanya doria ya kuwakamata vijana wa kata
hiyo baada ya kifo cha Mapunda.
Hata hivyo, Kyejo alisema hahusiki na tukio la kuwaita polisi wala doria na hata kifo cha kijana huyo hakuwa na taarifa nacho.
“Vijana
wameharibu mali nyingi za mtaa huu, ikiwamo kuvunjwa kwa meza za soko
na mali nyingine zilizokuwa sokoni hapo,” alisema Kyejo.
Kutokana na vurugu hizo, polisi wanadaiwa kuingilia kati kutumia nguvu ikiwamo kulipua mabomu.
Kwa
upande wake mama mdogo wa marehemu, Justina Kilasa, alisema marehemu
hakuwa na tabia mbaya, hivyo kitendo cha kukamatwa kwa madai ya kuhusika
na uhalifu sio cha kweli, kutokana na marehemu kuwa na tabia njema.
“Mwanangu
hakuwa mgomvi, alikuwa hajihusisha na tabia zozote mbaya, akitoka
kwenye kibarua chake cha kuuza machungwa kule Sido anaenda ibadani na
kurudi nyumbani,” alisema na kuongeza:
“Kwa kweli kifo hiki kimetushtua, mbaya zaidi Jeshi la Polisi limepiga mabomu ya machozi hapa msibani.”
Kilasa alisema kuwa mwili wa marehemu unahifadhiwa hospitali na wanasubiri kukabidhiwa kwa ajili ya maziko.
Mtendaji
wa Kata ya Iyela, Anna Supalika, alisema amesikitishwa na uharibifu
uliofanywa na vijana hao na kwamba hasara iliyopatikana haijabainika na
kwamba shughuli za kiofisi zimesimama.
Alipoulizwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alikiri kutokea kwa
tukio hilo na kwamba taarifa rasmi ataitoa baada ya uchunguzi
kukamilika.
0 comments:
Chapisha Maoni