Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anatarajiwa kusafirishwa nje ya nchi kwa matibabu mwezi mmoja kuanzia sasa.
Familia yake imesema Lissu baada ya kupata matibabu nje ya nchi amepanga kufanya mambo matano akirejea salama .
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 23, kaka wa Tundu Lissu,
Wakili Alute Mughwai alisema taratibu za kumsafirisha nje ya nchi
zimeanza.
Lissu,
ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu na mwanasheria mkuu wa chadema amelazwa
katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa
risasi zaidi ya 30 alipokuwa akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma
Septemba7.
"Awamu
ya tatu ya matibabu yake ni maalumu sana kwani itahusu pia mazoezi
ambayo kama haitafanyika vyema ataweza kupata ulemavu wa
kudumu,"alisema.
Hata
hivyo, alisema Lissu atapelekwa nje kwa ndege ya kawaida tofauti na
hali yake ya awali alipotakiwa kusafirishwa na ndege maalumu za
wagonjwa.
"Itatolewa
taarifa ni lini ataondoka kwa matibabu na atakwenda nchi gani, hasa
baada ya kupata ushauri wa mwisho wa madaktari katika hospitali
Nairobi," alisema.
Mughwai alisema amezungumza na Lissu akiwa Hospitali Nairobi na amemueleza kuwa akirejea tu nchini, kuna mambo makubwa matano ambayo atafanya.
Alisema
jambo la kwanza, ambalo atafanya ni kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma kuwashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa kuokoa
maisha yake siku aliyopigwa risasi.
Wakili
Mughwai alisema Lissu amemwambia baada ya hapo atakwenda kanisani na
msikitini kumshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yake kwa kufanya ibada
maalumu.
"Baada
ya ibada, tutaangalia utaratibu kifamilia kama itawezekana kwenda
kufanya matambiko kwenye makaburi ya wahenga wetu 76 waliofariki katika
vita miaka 200 iliyopita," alisema.
Alisema baada ya hapo, anatarajia kuendelea kufanya kazi zake za siasa na uwakili pale alipoishia kwa ari kubwa .
Wakili
Mughwai alisema jambo la tano atahakikisha anasimama na kupambana
kisheria na watu waliotaka kukatisha maisha yake baada ya kumpiga
risasi.
"Amesema
atahakikisha anasimamia jambo hili kwa uwezo wake wote ili kuhakikisha
wanafikishwa katika vyombo vya sheria waliohusika na uovu huo," alisema.
Familia yataka Lissu akahojiwe Nairobi
Akizungumzia
juu ya upelelezi wa shauri la Lissu, Mughwai alisema bado msimamo wao
upo palepale wanaomba wapelelezi kutoka nje ya nchi washirikiane na
wapelelezi wa ndani kuwakamata watuhumiwa.
Alisema
ingawa familia ya Lissu iliandika barua tangu Septemba 16, kutaka
wapelelezi wa kimataifa na kujibiwa na mwanasheria mkuu Septemba 20
kuwa jukumu la upelelezi ni la polisi.
"Tunataka
wapelelezi wa nje kushirikiana na wa ndani kwa sababu hatuna imani na
upelelezi kutokana na kasi ndogo kwani hadi sasa wamekuwa wakieleza
kukwama upelelezi kutokana na kutomuhoji dereva wa Lissu,"alisema.
Hata
hivyo, alisema kwa sasa Lissu anaweza kuongea mwenyewe hivyo, jeshi la
polisi linaweza kwenda Nairobi kumuhoji na atawapa maelezo yote ikiwepo
watu ambao aliwatambua.
"Bila shaka Lissu atawaeleza watu hao, walimshambulia kwa sababu gani,"alisema.
Familia yaelezea gharama
Katika
hatua nyingine, Mughwai alisema Oktoba 2, familia ya Lissu ilikutana na
viongozi wa bunge kujadili matibabu yake ambayo ni haki yake kisheria.
Alisema
baada ya mazungumzo hayo, Oktoba 8, familia iliandika barua rasmi kwa
katibu wa bunge kwa kuzingatia sheria ya bunge namba 14 kifungu cha 24
kuhusu stahiki za mbunge.
Alisema
barua hiyo, ilipelekwa bungeni kwa kutumia shirika la kubeba mizigo na
vifurushi la DHL na kupokelewa Oktoba 19 na baadaye aliwasiliana na
Spika Job Ndugai na kumweleza juu ya barua hiyo na aliahidiwa kuwa suala
hilo litashughuliwa.
Hata
hivyo, alisema familia haijapata mrejesho tangu wakati huo hadi Novomba
11, alipoamua kumpigia katibu mpya wa bunge baada ya kushauriwa na
Spika Ndugai ambaye aliahidi kufuatilia.
"Hivyo
hadi sasa bado Bunge halijaanza kugharamia matibabu ya Lissu kama
sheria inavyosema na Lissu amekuwa akitibiwa kwa michango ya watu mbali
mbali," alisema
Alisema
michango hiyo ambayo inakusanywa katika akaunti maalumu ya Chadema na
pia kupitia chama cha mawakili(TLS) ndio hadi sasa inatumika.
"Tutaendelea
kulitaka Bunge kugharamia matibabu kwani sio suala la hiari, ni haki ya
mbunge lakini pia tunaomba wananchi waendelee kuchangia matibabu ya
Lissu kupitia akaunti iliyotolewa na Chadema, chama cha TLS na kwa
familia"alisema
Akanusha mgawanyiko juu ya matibabu
Katika
hatua nyingine, Mughwai alisema, familia ya Lissu, Chadema na chama cha
Mawakili wa Tanganyika(TLS), hawana mgawanyiko wowote juu ya matibabu
ama hatua zinazoendelea za kumtibu Lissu.
Wakili
Mughwai alisema wanasikitishwa na taarifa kuwa familia imegawanyika juu
ya uamuzi wa kuliomba bunge kugharamia matibabu ya Lissu.
"Tupo
kitu kimoja wote familia yetu tupo pamoja kwa yote na Lissu anajua
hatua zote kwani hata makamishna wa bunge walipomtembelea Oktoba 23
aliwauliza kuhusu stahiki zake kama mbunge,"alisema.
Tundu
Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nje ya nyumba yake
akirejea kutoka vikao vya bunge Dodoma, Septemba 7 na kukimbizwa
hospitali ya Nairobi kwa matibabu ambapo hadi sasa anapatiwa matibabu.
0 comments:
Chapisha Maoni