Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amemkaribisha aliyekuwa mbunge
wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, ambaye amejivua
nyadhifa zote alizokuwa nazo CCM.
Akionyesha
kuwa na furaha leo Jumatatu wakati akiongea, Lowassa hakuwa na maneno
mengi, akiyafupisha kwa kusema “tumelamba dume”.
Nyalandu
(47), ambaye pia alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alitumia
nafasi hiyo kuomba kujiunga na Chadema, akisema anaiomba imfungulie
mlango.
Dakika
chache tangu Nyalandu aombe kujiunga na Chadema, Lowassa alimkaribisha
waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii huku akisema mwanasiasa
huyo amechelewa kujiunga na upinzani.
“Mbona
amechelewa? Alitakiwa awe amejiunga muda mrefu, tena hasa wakati wa
Uchaguzi Mkuu. Ninamkaribisha sana kwa sababu ni mwanasiasa mzuri na
anayejua majukumu yake,” alisema Lowassa ambaye alikuwa waziri mkuu wa
kwanza katika Serikali ya Awamu ya Nne.
“Nyalandu
ni hazina, ni mbunge imara na ni mwanasiasa wa mfano,” alisema Lowassa,
ambaye alijiunga na Chadema mwaka 2015 na kuwania urais kupitia
muungano wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa).
Lowassa
alimsifu Nyalandu kwa kuisaidia jamii na akatoa mfano jinsi
alivyosaidia watoto watatu wa Shule ya Lucky Vincent waliokwenda
kutibiwa Marekani baada ya kupata ajali ya basi iliyoua wanafunzi 32,
walimu wawili na dereva mmoja.
“Nyalandu
ana contacts (anafaham watu wengi) nyingi na jumuiya ya kimataifa, ni
bidhaa nzuri kuwanayo,” alisema Lowassa, ambaye katika uchaguzi wa urais
alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072,848 (asilimia 39.97)
ikiwa ni rekodi ya kura nyingi kwa upinzani tangu mfumo wa vyama vingi
urejeshwe mwaka 1992.
0 comments:
Chapisha Maoni