WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mradi ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi
II na kusema kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.
Amesema
hayo jana (Jumamosi, Julai 08, 2017) alipotembelea mradi huo wa
kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia unaojengwa eneo la Kinyerezi
jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu alisema kukamilika kwa mradi huo kutaliwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika, utakaowezesha kuendesha viwanda.
Alisema
mkakati wa Serikali ni kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme ili
Watanzania wapate umeme mwingi utakaosambazwa hadi vijijini kwa gharama
nafuu.
“Tunataka
tupate umeme wa kutosha ili viwanda vitakavyojengwa viwe na nishati ya
uhakika na ya gharama nafuu. Ni wajibu wetu kuendelea kuimarisha
utekelezaji wa miradi hii.” Alisema.
Naye,
Meneja wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi, Mhandisi Stephen Manda
alisema gharama za mradi wa Kinyerezi II ni dola milioni 344.
Meneja
huyo alisema tayari mradi huo umefikia asilimia 66.32 ya ujenzi wake na
sasa wako katika hatua mbalimbali za kukamilisha, ikiwemo ujenzi wa
misingi ya mitambo na jengo la kuendeshea mitambo.
“Pia
tunaendelea na ujenzi wa nguzo za kupokelea laini ya msongo wa kilovoti
220 kutoka Kinyerezi I hadi Kinyerezi II, ambapo mtambo wa kwanza wa
megawati 30 utawashwa ifikapo Desemba 2017 na kila mwezi tutaingiza
megawati 30 katika gridi ya Taifa.”
Alisema
miradi iliyoko katika eneo hilo ambayo iko katika hatua mbalimbali za
utekelezaji ni Kinyerezi 1 (150MW), Kinyerezi I Extension (185MW ) na
Kinyerezi II (240MW).
Mhandisi
Manda aliongeza kuwa mradi wa Kinyerezi 1 (150MW) ulikamilika Machi
2015 na miradi mwili ya Kinyerezi 1-extension na Kinyerezi II
inatarajiwa kukamilika mwaka 2018.
Mhandisi
Manda alisema miradi mingine inayotarajiwa kujengwa katika eneo hilo ni
wa Kinyerezi III (600 MW) na Kinyerezi IV utakaozalisha (450 MW).
Awali
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Sophia Mjema ambaye alimuwakilisha Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda alisema mradi huo umewanufaisha
wananchi wengi wa eneo hilo.
Alisema
hadi sasa wananchi 100 wa eneo la Kinyerezi wameajiriwa katika miradi
hiyo ambapo ni sawa na asilimia 40 ya watumishi wote.
Bi.
Sophia alisema mbali na ajira pia wananchi wa eneo hilo watanufaika kwa
kuboreshewa huduma mbalimbali za kijamii katika eneo hilo zikiwemo za
maji na elimu ambapo wameahidiwa kupewa madawati ya shule tano
0 comments:
Chapisha Maoni