Bunge
limepitisha sheria mpya ambayo sasa itatambua haki na dhamana ya
serikali katika makinikia ambayo itakuwa ni marufuku kuchenjuliwa nje ya
nchi na serikali itashiriki kwa asilimia kuanzia 16 hadi 50 katika
shughuli zote za uchimbaji, uchakataji na uchejuaji madini na ununuzi wa
hisa katika kampuni ya uchimbaji madini.
Aidha, Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) umefutwa rasmi na sasa kunaanzishwa Kamisheni ya Madini, na kwamba kuanzia sasa umiliki wa leseni mbalimbali zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini, hautahamishwa kabla haujafanyiwa uendelezaji katika kitalu husika.
Akielezea
mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa
Mwaka 2017 katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, Waziri wa Katiba na
Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema asilimia hizo za hisa ni kwa
kuangalia thamani ya gharama ambazo serikali inahamia katika vituo vya
uwekezaji na kodi aliyopewa mwekezaji.
Profesa
Kabudi alisema muswada huo pia unatambua haki na dhamana ya serikali
juu ya makinikia na kuweka utaratibu wa kuyahifadhi sehemu maalumu
migodini chini ya uangalizi wa serikali.
“Kupitia
marekebisho hayo, makinikia yanayotolewa nchini bila kufanyiwa
uchunguzi wa kupata thamani halisi kabla ya kuchenjuliwa na uchenjuaji
utafanyika nchini. Kuanzia sasa makinikia hayatauzwa nje ya nchi,
yatauzwa kwenda kwa wachenjuaji wa ndani ya nchi yakiwa ni bidhaa ambayo
itatozwa kodi,” alifafanua.
Alisema
pia muswada unaipa serikali haki na dhamana juu ya usimamizi wa bidhaa
zote na maliasili, zinazotokana na uchimbaji, uchakataji na uchejuaji wa
madini yakiwamo makinikia au kwa jina maarufu mchanga wa dhahabu.
Aidha,
alisema muswada umelenga kutambua na kuweka chini ya uangalizi wa
serikali maeneo yote ya uchimbaji na madini kwa lengo la kuweka ulinzi
na usimamizi madhubuti wa madini kwa lengo la kuweka ulinzi na usimamizi
madhubuti wa maeneo ya uchimbaji.
“Hii
itasaidia kuwepo ulinzimahsusi wa maeneo yote ya uchimbaji wa madini,
kuwepo kwa utaratibu wa serikali kufanya ukaguzi na udhibiti wa
usambazaji wa madini, kuipa serikali uwezo wa kudhibiti na kutambua
viwango vya madini yote yanayotolewa kwenye maeneo ya migodi na kupitia
vyombo vya ulinzi na usalama vya serikali,” alieleza.
TMAA yazikwa rasmi
Alieleza
kuwa kufutwa kwa TMAA kunatokana na majukumu yake, yaliyokuwa
yakitekelezwa na wakala huyo kuhamishiwa kwa Kamisheni ya Madini ambayo
itaanzishwa.
Akiwasilisha
muswada huo, Profesa Kabudi alisema kutokana na kufanyiwa mapitio ya
madaraka ya Waziri na Kamishna wa Madini kwa lengo la kuwapunguza baadhi
ya majukumu na madaraka yatahamishiwa kwa Kamisheni ya Madini.
Alisema
kamisheni inayopendekezwa kuanzishwa itakuwa na jumla ya makamishina
tisa, na watu kati yao akiwamo Mwenyekiti watakuwa wa kudumu.
“Watashirikiana
na watendaji wakuu kutekeleza majukumu yao ya Kamisheni ya kila siku,
makamishna wengine watakuwa wa muda na watakutana katika vikao maalumu
vya kamisheni kwa ajili ya kufanya maamuzi ya misingi na kufuatilia
utekelezaji wake,” alifafanua na kuongeza kuwa makamishina wa muda
watateuliwa kutokana na nafasi zao ambao ni Katibu Mkuu Hazina, Katibu
Mkuu Tamisemi, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Ulinzi
na Katibu Mkuu Ardhi.
“Kamisheni
inayopendekezwa kuundwa itachukua majukumu sehemu kubwa ya majukumu ya
Kamishna wa Madini kwa sasa. Majukumu hayo ni pamoja na kutoa, kuhuisha
au pale itakapolazimika kufuta leseni zote zinazotolewa kwa mujibu wa
sheria ya madini, kusimamia shughuli za madini ikiwa ni pamoja na
kufanya ukaguzi maeneo ya migodi.
"Pia
majukumu yote yaliyokuwa yakitekelezwa na TMAA yatahamishiwa na kuwekwa
chini ya Kamishna. Na kwa msingi huu TMAA inafutwa,” alibainisha.
Umiliki wa leseni
Kuhusu kutohamisha leseni, alisema hatua hiyo ni katika kuzuia watu kufanya biashara ya udalali wa leseni.
Kuhusu kutohamisha leseni, alisema hatua hiyo ni katika kuzuia watu kufanya biashara ya udalali wa leseni.
“Katika
kuweka masharti yanayokusudia kuzuia watu kufanya biashara ya udalali
wa leseni mbalimbali zinazotolewa kwa mujibu wa sheria ya madini,
mmiliki wa leseni hataruhusiwa kuhamisha umiliki wa leseni kabla ya
uendelezaji katka kitalu husika,” alieleza.
Aliongeza, “baada
ya kumalizika kwa muda wake, leseni itahuishwa kwa kipindi kimoja tu,
na baada ya hapo umiliki wa kitalu husika utarejeshwa serikalini.”
0 comments:
Chapisha Maoni