Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angellah Kairuki,
amesema katika mwaka huu mpya wa fedha watumishi wa umma watakuwa
wanalipwa mishahara kwa wakati mmoja ili kupunguza matatizo ya mishahara
yanayojitokeza.
Kairuki
ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Julai 18 wakati akizungumza na watumishi
wa wilaya mpya ya Ubungo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake aliyoianza
jana katika halmashauri hiyo.
Amesema
awali watumishi hao walikuwa wanapata mishahara yao kwa nyakati tofauti
lakini sasa wataingizia mishahara yao moja kwa moja katika akaunti ya
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) badala ya kupitia benki za biashara.
"Hatutaki
itokee huyu amewekewa mshahara tarehe 27, huku mwingine akienda
kuangalia salio katika akaunti anaambiwa bado lakini sasa hivi itakuwa
wakati mmoja," amesema Kairuki huku akishangaliwa na watumishi wa halmashauri hiyo.
Alisisitiza
lengo la kuweka mfumo huo ni kuhakikisha watumishi wote wanapata
mshahara wao wakati mmoja na hiyo itasaidia Serikali kusimamia kwa
umakini mishahara.
Amefafanua
kwamba siku tatu kabla mshahara haujaingizwa katika akaunti ya
mtumishi, mwajiri sekta husika atapelekewa orodha ya watumishi
watakaotakiwa kulipwa mishahara.
"Matumaini yangu waajiri watakuwa makini kuangalia orodha hizo ili isitokee hata mtumishi mmoja akaachwa," anasema Kairuki.
0 comments:
Chapisha Maoni