Mkurugenzi
wa Mashtaka (DPP) ameshinda rufaa dhidi ya viongozi wa Jumuiya ya
Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi
Ahmed na wenzake 21 wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu.
DPP
alikata rufaa Mahakama ya Rufaa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kuhusu
mamlaka ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza na kutoa uamuzi
wa hoja walizoziibua washtakiwa kupitia kwa mawakili wanaowatetea, baada
ya kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Siku
waliposomewa mashtaka, washtakiwa kupitia mawakili, Juma Nassoro na
Abubakar Salim pamoja na mambo mengine walihoji uhalali wa Mahakama ya
Kisutu kusikiliza shauri lao, pia waliiomba mahakama iwafutie mashtaka
wakidai kulikuwa na kasoro za kisheria.
Mahakama
ya Kisutu katika uamuzi wake ilikataa kusikiliza hoja za washtakiwa
hao, ikisema haina uwezo wa kisheria kusikiliza hoja zozote kutoka kwao
kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yanasikilizwa na Mahakama Kuu tu, hivyo
ikawaelekeza kuwasilisha hoja hizo Mahakama Kuu.
Washtakiwa
hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, hivyo walifungua maombi
ya mapitio Mahakama Kuu, wakiiomba mahakama iitishe na kuchunguza
kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo ili kujiridhisha na uhalali na
usahihi wake.
Walidai Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kusikiliza na kutoa uamuzi wa hoja walizoziibua baada ya kusomewa mashtaka.
Mahakama
Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Fauz Twaib ilikubali hoja za
mawakili wa washtakiwa kuwa Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kusikiliza
na kutoa uamuzi wa hoja zao na alielekeza mahakama hiyo kuendelea na
usikilizwaji wa uamuzi wa hoja za washtakiwa hao.
DPP hakuridhika na uamuzi huo hivyo alikata rufaa Mahakama ya Rufaa, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Mahakama
ya Rufaa katika hukumu iliyoandikwa na Jaji Bethuel Mmila kwa niaba ya
wenzake, Jaji Kipenka Mussa na Jaji Rehema Mkuye waliounda jopo
lililosikiliza rufaa hiyo, imetengua uamuzi wa Mahakama Kuu.
Hukumu
hiyo imesomwa leo na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa,
Phocus Bampikya ikisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina uwezo wa
kusikiliza na kuamua hoja zilizoibuliwa na washtakiwa hao kupitia kwa
mawakili wao.
Mahakama
ya Rufaa imesema hakuna sharti lolote kisheria linaloipa mamlaka
mahakama hiyo kusikiliza na kutoa uamuzi wa hoja hizo na kwamba,
mahakama hiyo ina uwezo wa kuwezesha mshtakiwa/washtakiwa kusomewa au
kuwezesha kusomewa maelezo ya mashahidi tu kabla ya kwenda kusikilizwa
na Mahakama Kuu.
Imesema
manufaa ya matakwa hayo ya mahakama kuwezesha mshtakiwa kusomewa
maelezo ya mashahidi ni kuwafanya kujua mapema aina ya ushahidi
utakaotolewa dhidi yake wakati wa usikilizwaji Mahakama Kuu na
watakaotoa ushahidi huo ili kupata nafasi nzuri ya kuandaa utetezi wake.
“Ni
mtazamo wetu kwamba mambo/hoja zilizoibuliwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu ni za kisheria ambazo Mahakama ya Hakimu Mkazi haina
mamlaka kuyaamua. Masuala hayo yanapaswa kusubiri na kuibuliwa Mahakama
Kuu wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo,” inasema hukumu hiyo.
Mahakama
hiyo imeelekeza Mahakama ya Kisutu kuendelea na shauri hilo kuanzia
pale lilipokuwa limeishia kabla ya kufunguliwa kwa mapitio Mahakama Kuu.
0 comments:
Chapisha Maoni