Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Vincent
Mashinji pamoja na viongozi watano wa chama hicho wakiwemo wabunge
wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Ruvuma, wakikabiliwa na
makosa mawili ikiwemo kufanya mkusanyiko uliotishia usalama wa nchi.
Dk
Mashinji alifikishwa mahakamani hapo jana na wanachama wengine watano
wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Polisi wa Kituo Kikuu cha Polisi
Songea Mjini.
Walisomewa
mashitaka mawili ya kufanya mkusanyiko usio halali na kufanya
maandamano kinyume cha sheria, ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa
nchi.
Akisoma
mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Ruvuma,
Simon Kobelo, Wakili Mfawidhi wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Kanda ya Songea, Renatus Mkude alidai Julai 15, mwaka
huu mjini Mbamba Bay wilayani Nyasa, washitakiwa walikamatwa na Polisi
wakiwa katika maandamano bila kuwa na kibali.
Aidha, Mkude alifafanua kuwa kosa lingine ni kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria, hivyo kuhatarisha usalama wa nchi.
Katika
kesi hiyo ya jinai namba 113 ya mwaka 2017, mbali na Dk Mashinji,
washitakiwa wengine ni wabunge Zubeda Sakuro wa Viti Maalumu na
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini Masasi na mbunge wa Ndanda kupitia
chama hicho, Cecil Mwambe.
Wengine
ni Katibu wa Ulinzi wa Taifa wa Chadema, Sanuda Madawa, Katibu Mwenezi
Kanda ya Kusini Masasi, Charles Makunguru na Katibu wa Chadema Kanda ya
Kusini Masasi, Filbert Ngatunga.
Washitakiwa baada ya kusomewa mashitaka yao, walikana kutenda makosa hayo.
Hata
hivyo wakati wanasheria wa Chadema wakikamilisha taratibu ya dhamana,
Jeshi la Polisi liliwachukua washitakiwa na kuwapandisha kwenye gari na
kuwapeleka rumande hadi kesho, ambapo kesi hiyo itatajwa tena.
DK
Mashinji na wanachama hao walikamatwa Julai 15, mwaka huu katika mji
mdogo wa Mbamba Bay wilayani Nyasa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyasa
wakiwa katika maandamano na kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria, licha
ya serikali kuzuia mikutano yote vyama vya siasa.
Baada
ya washitakiwa hao kushikiliwa na polisi wilayani Nyasa kwa saa 48,
walipata dhamana kabla ya Jumanne na kupelekwa Ofisi ya Kamanda wa
Polisi Mkoa mjini Songea, kabla ya jana kufikishwa mahakamani kujibu
tuhuma hizo.
Upande
wa utetezi ukiongozwa na Wakili Edson Mbogoro ulilalamikia kitendo cha
wateja wao, kupelekwa mahabusu kwani hakimu tayari alishatoa ruhusa ya
dhamana kwa washitakiwa, jambo ambalo alisema ni kinyume cha taratibu.
0 comments:
Chapisha Maoni