Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana
tarehe 28 Juni, 2017 amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme
na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri
Mkuu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn kwa lengo la kubadilishana
uzoefu na Tanzania.
Mhe.
Rais Magufuli alisema timu hiyo inayoongozwa na Waziri wa Maji,
Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dkt. Seleshi Bekele imekuja nchini
kubadilishana uzoefu na timu ya wataalamu wa Tanzania ambayo inasimamia
utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya
mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).
Katika
mazungumzo na timu hiyo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe.
Rais Magufuli alielezea nia yake ya kuhakikisha mawazo ya Baba wa Taifa
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya tangu mwaka 1980 juu ya
kuzalisha umeme kutoka maporomoko ya mto Rufiji, yanatekelezwa haraka
iwezekanavyo.
“Sasa
hivi nchi yetu inazalisha megawatts 1,450 tu, lakini Stiegler’s Gorge
itatuzalishia megawatts 2,100 umeme huo ni mwingi na utatusaidia katika
viwanda, hivyo Serikali tumeamua kutekeleza mradi huu.
“Najua
kutaanza kutokea vipingamizi mbalimbali, lakini naomba Watanzania tuwe
na sauti moja, eneo litakalotumia ni Kilometa za mraba 1,350 ambalo ni
sawa na asilimia 3 tu ya eneo lote la hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa
Kilometa za mraba 45,000” alisema Mhe. Rais Magufuli na kuongeza
kuwa mradi huo utakuwa na faida nyingi zikiwemo uvuvi, maji kwa ajili ya
wanyamapori na kilimo.
Kwa
upande wake Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dkt.
Seleshi Bekele alisema Ethiopia ambayo kwa sasa inazalisha megawatts
4,300 za umeme kwa kutumia maji, inayo miradi mingi ya kuzalisha umeme
kwa kutumia maji ambayo itaiwezesha kufikia uzalishaji wa megawatts
17,000 ifikapo mwaka 2020 na kwamba yeye na watalaamu wa nchi wapo
tayari kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya umeme na
ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme.
Mazungumzo
hayo yalihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi,
Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania Dkt. Medard Kalemani na
timu ya wataalamu wa Tanzania wanaosimamia utekelezaji wa ujenzi wa
mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya mto Rufiji
(Stiegler’s Gorge Power Project).
0 comments:
Chapisha Maoni