Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kulipa faini ya Sh200 milioni
mfanyabiashara, Ndama Shabani Hussein maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto
ya Ng’ombe baada ya kulikubali na kutiwa hatiani katika shtaka la sita
la kutakatisha dola za Marekani 540,000.
Akitoa
hukumu hiyo jana Ijumaa, Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa amesema
endapo mshtakiwa huyo atashindwa kulipa kiasi hicho cha fedha atatumikia
kifungo cha miaka mitano jela.
Hukumu
hiyo ya shtaka la sita la kutakatisha fedha ilitolewa baada ya Wakili
wa Serikali, Christopher Msigwa kumsomea maelezo ya awali (PH) Ndama na
kuyakubali maelezo yote yanayounda shtaka hilo la kutakatisha fedha,
akapatikana na hatiani na kupewa adhabu hiyo.
Kabla
ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Msigwa aliiambia Mahakama kuwa
mshtakiwa amekubali shtaka la sita la kutakatisha fedha na maelezo
yanayounda shtaka hilo.
“Hatuna
kumbukumbu za nyuma za makosa dhidi ya Ndama ila ni rai ya upande wa
mashtaka kuwa wakati mahakama ikitoa adhabu izingatie matakwa ya kifungu
cha 13(a) cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha,” imesema hati ya hukumu.
Alisema
pia mahakama ibebe dhana ya sheria hiyo ambayo lengo lake ni kuzuia
makosa ambayo yanalenga kudidimiza uchumi wa nchi na uzito wa kosa
ambalo mshtakiwa amelifanya.
Kwa
upande wa Wakili Wabeya Kung’e anayemtetea mshtakiwa huyo kwa
kushirikiana na Jeremiah Mtobesya, Kung’e aliiambia mahakama kuwa ni
wazi mshtakiwa amekiri kosa baada ya kusomewa maelezo ya awali hivyo
mahakama isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa.
Aliiomba
mahakama izingatie maombi yao kwa sababu mshtakiwa huyo hilo ndiyo kosa
lake la kwanza, kitendo chake cha kukiri kosa kinaonyesha kusikitikia
kosa alilolitenda na kwamba anayo familia ambayo inamtegemea ambao kwa
kipindi cha mwaka mmoja ambacho amekaa ndani imepata shida kwa kukosa
huduma yake.
“Kwa
kuzingatia kifungu cha 13(a) cha sheria ya kutakatisha fedha ni rai
yetu mahakama tukufu isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa sababu
amejutia kosa alilolitenda,” alisisitiza Kung’e. Hivyo Ndama
alihukumiwa kulipa faini ya Sh 200 milioni ama akishindwa kutumikia
kifungo cha miaka mitano jela.
Juni
6, 2017 Ndama aliiomba mahakama akumbushwe shtaka, akakumbushwa na
Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson na akalikubali shtaka hilo.
Akisomewa
maelezo ya awali mahakamani hapo, Ndama alikubali maelezo ya awali
aliyosomewa ikiwamo nyaraka zilizotumika kufungua akaunti iliyotumika
kuingizwa fedha hizo, hundi 18 zilizotumika kutolea fedha hizo, maelezo
ya benki ‘bank statement’ na Swift massage.
Iwapo
atakamilisha kulipa Sh200 milioni atakuwa huru kuendelea katika
mashtaka matano mengine yanayomkabili mahakamani hapo ambayo upelelezi
wake bado haujakamilika.
Ndama
anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na atoe fedha taslimu
kiasi cha Dola za Marekani 270,200 ambacho ni sawa na zaidi ya Sh600
milioni mahakamani hapo na mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi
hicho cha fedha.
0 comments:
Chapisha Maoni