BAADHI
ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, wamesema
tatizo la upungufu wa walimu kwenye shule za msingi zilizopo vijijini
kunachangiwa na walimu hasa wa kike kutaka kufundisha mjini.
Walisema
baadhi ya walimu wa kike wamekuwa wakighushi vyeti vya ndoa ili
kuonesha wameolewa na kuwafuata waume zao mijini jambo linalozorotesha
jitihada za Serikali kumaliza tatizo la walimu kwani baadhi ya shule za
vijijini zina walimu hadi wawili.
Madiwani
hao waliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye Kikao cha Baraza la
Madiwani wa halmashauri hiyo ambapo Diwani wa Kata ya Lusanga, Sesiwa
Mhando, alidai halmashauri ilitenga sh. milioni 30 kwa ajili ya walimu
kupelekwa shule za vijijini; lakini hadi sasa hajui mchakato huo
umekwamia wapi.
"Tatizo
la walimu kwenye shule za msingi linatokana na walimu kujazana mijini
hasa wa kike wakiwa na ndoa bandia, madiwani tulitenga sh. milioni 30
ili zitumike kupeleka walimu vijijini lakini sijui mchakato huo umeishia
wapi," alihoji.
Kwa
upande wake, Kaimu Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani humo,
Stuart Kuziwa, alisema tatizo la walimu ni la kitaifa likiwemo la
kujazana mijini lakini hata shule zilizopo mjini nazo zina upungufu wa
walimu.
"Hata
shule za mjini nazo zina upungufu wa walimu, tumeomba kupatiwa walimu
230 kwa miaka mitatu mfululizo, hilo linaweza kumaliza shida ya walimu
katika shule za msingi," alisema.
Diwani wa Kata ya Bwembera, Kapteni mstaafu Tito Haji, alisema moja ya shule za msingi kwenye kata yake ina walimu wawili.
"Kwenye
Kamati ya Fedha,mlidai tatizo la walimu limekwisha sasa iweje leo
mnatueleza kuwa tatizo la walimu bado lipo Muheza, Shule ya Msingi
Msowelo ina walimu wawili lakini mjini walimu wamejaa," alisema Kapteni Tito.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Amir Kiroboto, alisema madiwani
wasilalamikie tatizo la walimu kujaa mijini bali waangalie idadi ya
wanafunzi kwani shule nyingi za mjini zina wanafunzi wengi.
0 comments:
Chapisha Maoni