Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimepinga kusudio la Mamlaka ya
Nishati na Maji (Ewura) la kuipa leseni Kampuni ya kufua umeme ya
Independent Power Limited (IPTL).
LHRC
imetangaza kuweka kusudio la kupinga IPTL kupewa leseni ya kuendelea
kuliuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), huku wakihoji usafi
na makandokando dhidi ya kampuni hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
LHRC, Anna Henga, alisema kwa sasa wanamalizia kuandaa pingamizi lao la
kisheria ambalo wataliwasilisha Ewura.
Henga
alisema IPTL haina sifa tena ya kuendelea kuuza umeme nchini, hasa
baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha kupitia
Akaunti ya Tegeta Escrow.
Alisema
mwaka 2014 Bunge kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
ilitoa mapendekezo mbalimbali juu ya umiliki wa mitambo ya IPTL.
“Suala
hili tumekuwa tukilifuatilia tangu zamani na tuna ushahidi kwamba IPTL
haipaswi kupata tenda hii kwa kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Bunge
kuhusu kampuni hii bado hayajatekelezwa.
“Tutapeleka
maoni yetu Ewura, tutawaandikia jinsi tunavyoona, lakini kwa hali ya
kawaida kwa IPTL hawakuhitaji hata kuomba maoni ya wananchi katika
kufanya uamuzi kwa kuwa sifa mojawapo ya kupatiwa leseni ni uadilifu wa
muhusika,” alisema Henga.
Alisema
moja ya mapendekezo yaliyotolewa na iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC) katika Bunge la 10, hadi sasa hayakutekelezwa,
ikiwamo kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania
(Takukuru), kufanya uchunguzi juu ya umiliki na uwepo wa rushwa katika
utendaji kazi wa IPTL na wabia wake.
Henga alisema hadi sasa bado hakuna taarifa sahihi juu ya upotevu wa fedha za Watanzania katika akaunti ya Escrow.
“Je,
Ewura inatuaminisha kuwa hatuna tatizo na IPTL je, IPTL wapo peke yao
walioomba, hakuna kampuni nyingine ya kuwapa? Na kama hamna, wanaweza
kutoa sababu za kuwapa IPTL waendelee na leseni hiyo?” alihoji Henga.
Pia
alishangazwa na hatua ya uwazi wa kuhitaji maoni kwa kampuni hiyo, hali
ya kuwa mikataba inaingiwa kwa siri baina ya wadau hao na Serikali.
“Tumeshangazwa
na kitendo cha Ewura kutaka maoni ya wadau, huku ikiwa inafahamu fika
kuwa mikataba kati ya Serikali na IPTL ni siri na hivyo wadau hawana
sababu ya kimkataba za kutoa pingamizi au maoni,” alisema Henga.
Alisema
kutokana na sababu hizo zinazoendana na misingi ya uwajibikaji, LHRC
inapendekeza na kuishauri Ewura kusitisha mara moja kusudio la kukusanya
maoni ya kuongezea muda kampuni hiyo hadi Serikali itakapotekeleza
mapendekezo ya Bunge.
LHRC
imeitaka Ewura kuomba radhi Watanzania na wabunge kwa kujaribu
kuirudisha IPTL kwa jamii, huku ikitambua wazi kuwa miaka mitatu
iliyopita ilikuwa katika kashfa na mtafaruku ndani na nje ya Tanzania.
Kituo
hicho kimeitaka jamii na Watanzania kwa ujumla, wakiwamo wabunge,
viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi wa kawaida kuungana kwa
masilahi ya umma kwa kuwasilisha mapingamizi kwa wingi ili kugomea
mpango wa IPTL kupewa leseni ya kuuza umeme.
Hata
hivyo Kampuni hiyo huenda ikakosa leseni kutokana na msimamo wa
Serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kwa kupinga
mikataba mibovu ya kinyonyaji kwa taifa.
0 comments:
Chapisha Maoni