test

Jumamosi, 20 Mei 2017

Watuhumiwa wa Mauaji Kibiti Watiwa Mbaroni




Mkuu  wa Wilaya ya Rufiji, ambaye pia anakaimu Wilaya ya Kibiti, Juma Njwayo,  amesema vyombo vya dola vimewakamata watu wengi wanaodaiwa kuhusika na uhalifu wa kuua watu katika maeneo mbalimbali ya wilaya hizo.
 
Njwayo amesema licha ya watuhumiwa hao kukamatwa, pia vyombo vya dola vinaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaojihusisha na vitendo hivyo.

“Kuna watu wanaoshukiwa ambao ni wengi wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa, kuna wengine wanatafutwa na wakipatikana watahojiwa, lakini hawajakamatwa kwa maana ya kwamba imethibitika wao ni wahalifu,” alisema.

Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi wa maeneo hayo waendelee kufanya shughuli zao, lakini kwa tahadhari.

“Watu wanalima, wanaofanya shughuli za Serikali wanafanya, lakini haya yanafanyika tunapata uthibitisho kwa mfano wa hawa watu wanne waliouawa huku Rufiji, kwa hiyo hali iko hivyo. Tunaomba watu sasa wafanye shughuli zao kwa tahadhari, wakiona mtu wasiyemjua watoe taarifa katika vyombo.

“Pia kama wanazo taarifa watuambie, sisi tunajua hawa watu wako kwenye jamii, haiwezekani mtu asiyekujua wewe aje akupige risasi jioni, lazima awe anakujua na kama hakujui basi anashirikiana na mtu anayekujua. Hivyo tunawasisitiza hawa wananchi wetu wawe na tahadhari ya kiusalama,” alisema.

Alipoulizwa amebaini nini katika matukio hayo yanayowalenga zaidi viongozi wa Serikali, alisema suala hilo ni gumu na bado haijajulikana sababu ya uhalifu huo.

“Hatujui sababu ni nini, lakini ni kweli watu wote waliopata hilo tatizo wapo askari, wapo viongozi ama ni wa serikali ya vijiji au chama tawala,” alisema.

Awali, Njwayo alikiri wazi kuwa wananchi katika maeneo hayo wanaishi kwa hofu kwa sababu matukio si ya kawaida.

“Lazima uhofu, yaani upo nyumbani kwako unakula mtu anakuja anakupiga risasi, watu nao wanasikia mlio wa risasi lazima wapate hofu, hilo ni jambo la kila mtu mwenye akili yake timamu lazima ahofie.

“Lakini sisi kwa upande wetu wa wilaya halitupendezi jambo hili, tuna hatua nyingi tunazichukua kwa kushirikiana na Serikali Kuu kupambana na jambo hili,”
alisema.

Kauli ya Njwayo imekuja siku chache baada ya watu wasiofahamika kumuua Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kijiji cha Muyui, Iddy Kirungi, huku mtoto wake, Nurdin Kirungi, akipigwa risasi ya tumbo wilayani Kibiti.

Wauaji hao baada ya kutekeleza unyama huo walitokomea kusikojulikana, hali inayotishia usalama wa raia na mali zao, huku wengine wakilazimika kuzikimbia nyumba zao kwa hofu ya kupoteza maisha.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema linaendelea kuwasaka wahalifu na kuimarisha ulinzi.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni