Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco) limezungumzia tozo ya asilimia 1.1
wanayokatwa wateja baada ya kununua umeme kwa njia ya mitandao ya simu
na kupitia kwa mawakala wa benki.
Utaratibu
huo ulianza Aprili 2 baada ya mfumo wa malipo wa Tanesco kuunganishwa
na ule wa Serikali (GePG) ambao utawalazimu wateja wa huduma hiyo
kulipia gharama za miamala husika, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo
huduma hiyo ilikuwa ikitolewa bure.
Akizungumza
jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema kuwa bei
ya umeme bado haijapanda iko palepale kama ilivyokuwa awali.
“Hizi
taarifa za kupanda kwa gharama za umeme siyo za kweli, hatuwezi kufanya
hivyo kwa sababu bei ilipitishwa na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji), hivyo hatuwezi kupandisha bila wao
kuridhia,” alisema Dk Mwinuka.
Alisema tozo baada ya kununua umeme si kitu cha ajabu kwani watu wa mitandao hawawezi kumfanyia mtu huduma bila kuigharamia.
Meneja
Masoko wa Tanesco, Mussa Chowo alisema utaratibu uliopo siyo mpya kwa
kuwa kulikuwa na mkataba baina ya Serikali na mitandao ya simu kuwa na
tozo kwa anayenunua kwa njia ya simu.
Alisema
sehemu ambayo mteja atanunua umeme bila tozo ni ofisi za Tanesco, Benki
ya NMB na CRDB, lakini kama watanunua kwa wakala wa benki watatozwa
asilimia 1.1.
Alisema
mteja akinunua umeme wa Sh5,000 atachajiwa Sh55 na atakayenunua umeme
wa Sh10,000 atatozwa Sh110 na umeme wa Sh100,000 atatozwa Sh1,100.
0 comments:
Chapisha Maoni