SERIKALI imewaonya wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutowaozesha watoto wote wa kike waliohitimu darasa la saba mwaka huu wakati wa kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao, iwe ni kwa sababu yoyote ile au kwa lengo la kujipatia mali kwa njia ya mahari.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mkono wa serikali kisheria ni mrefu, hivyo wazazi au walezi watakaokwenda kinyume watahakikisha kuwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Ummy ameyasema hayo jana katika tamko maalumu alilolitoa kwa wanafunzi hao waliohitimu elimu ya msingi nchini kote.
Alisema wazazi na walezi wanapaswa kutambua umuhimu wa mtoto wake kuendelea kielimu, na kukua kimwili na kiakili kabla ya kuingia katika ndoa kwani elimu ya watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza umaskini katika mataifa yanayostawi.
“Natoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika za Serikali za Mtaa, Kijiji, Kata, Wilaya na hata katika Madawati ya Jinsia na Watoto yaliyopo Polisi, pale watakapobaini mzazi au mlezi au taasisi anaenda kinyume na jitihada za serikali za kumuendeleza mtoto kielimu hasa katika kudhibiti ndoa za watoto waliomaliza Elimu ya Msingi hususan katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao,” alisema Ummy.
Aidha, amewataka wahitimu wa darasa la saba waliomaliza mitihani yao juzi, kutojihusisha na tabia au vitendo vyovyote vinavyohatarisha afya, usalama na maendeleo yao.
Takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi 795,761 (wavulana 372,883 sawa na asilimia 46.86 na wasichana 422,878 sawa na asilimia 53.14) walisajiliwa na kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu.
“Hivyo ningependa kutumia fursa hii kuwaasa watoto waliomaliza darasa la saba kutojihusisha na tabia au vitendo vyovyote vinavyohatarisha afya, usalama na maendeleo yao, kama vile kujihusisha kwenye masuala ya ngono, matumizi ya dawa za kulevya na vileo katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo ya mitihani yao,” alisema Ummy.

