Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 28 Mei, 2017 amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya
Mwaisela iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwashukuru
Madaktari na Wauguzi kwa juhudi kubwa wanazofanya kunusuru maisha ya
watu.
Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamewatembelea wagonjwa hao majira ya saa moja ya asubuhi wakitokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambako wamehudhuria ibada ya Jumapili.
Miongoni
mwa wagonjwa waliojuliwa hali na Mhe. Rais Magufuli na mkewe ni Mzee
Francis Maige Kanyasu (Ngosha) aliyelazwa katika chumba namba 310 na
Mtoto Shukuru Musa Kisonga aliyelazwa katika chumba namba 312 ambaye
hivi karibuni aliripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika uliosababisha
aishi kwa kunywa mafuta ya kula, sukari na Maziwa.
Pamoja
na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mwaisela na
kuwashukuru Madaktari na Wauguzi, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali
itaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali
hiyo na changamoto zinazowakabili madaktari na wauguzi.
“Jamani,
Madaktari tunawashukuru sana, mnafanya kazi nzuri, Madaktari wote
nchini pokeeni pongezi zangu, sisi Serikali tutaendelea kuzikabili
changamoto hizo na siku moja zitakwisha, kikubwa ni kumtanguliza Mungu
mnapofanya kazi ya kuokoa maisha ya watu kwa juhudi kubwa, mnafanya kazi
ya Mungu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof.
Lawrence Museru amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwatembelea wagonjwa
katika hospitali hiyo na amemhakikishia kuwa Madaktari tayari
wamegundua magonjwa yanayowakabili Mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha)
na Mtoto Shukuru Musa Kisonga na kwamba wanaendelea vizuri na matibabu.
Aidha,
Prof. Museru amesema hospitali hiyo imepiga hatua kubwa ya kujenga
uwezo wa kutibu magonjwa ambayo wagonjwa walilazimika kwenda kutibiwa
nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha nyingi za Serikali.
“Mhe.
Rais hospitali yetu sasa imeanza kufanya upasuaji na kutoa tiba ya
magonjwa ambayo yalilazimu wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, mfano
hivi sasa tunatoa huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa takribani 250,
na kuanzia mwezi Julai mwaka huu tutaanza kupandikiza figo.
“Huduma
hii hugharimu kati ya Shilingi Milioni 60 na Shilingi Milioni 70 kwa
mgonjwa mmoja anayekwenda kutibiwa nje ya nchi, lakini hapa nchini
gharama zinashuka hadi Shilingi Milioni 21” amesema Prof. Museru.
Prof.
Museru ameongeza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili pia inajipanga
kuanza kutoa huduma ya matibabu kwa watoto wenye matatizo ya usikivu
ambao wapo hatarini kuwa viziwi na hivyo kuokoa fedha nyingi
zinazotumika kuwatibu nje ya nchi, kutoka Shilingi Milioni 90 hadi
Shilingi Milioni 30.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
pamoja na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakimjulia hali Mzee Francis Maige
Kanyasu(Ngosha) aliyelazwa Wodi ya Mwaisela katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kwa ajili ya Matibabu. Wakwanza kushoto ni Mkurugenzi wa
Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Lawrence Museru
pamoja na Dkt. Juma Mfinanga Daktari Bingwa wa magonjwa ya Dharura na
Ajali katika hospitali hiyo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na Mzee Francis Maige Kanyasu(Ngosha) aliyelazwa Wodi ya Mwaisela
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya Matibabu
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
pamoja na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakimjulia hali mtoto Shukuru
Kisonga aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mtoto Shukuru
alikuwa akidaiwa kuishi kwa kula Sukari, Maziwa na mafuta ya kula
lakini hali yake imeimarika zaidi na kuanza kula vyakula vya kawaida.
Katikakati ni Mama yake Shukuru Mwanahabibi Mohamed Mtei.
0 comments:
Chapisha Maoni