Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Shirikisho la Taifa
la Utengenezaji wa Mitambo ya Viwanda la China (China National
Machinery Industry Federation – CNMIF) kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
itawapa ushirikiano wa kutosha katika mpango wao wa kuwekeza katika
uzalishaji wa nishati ya umeme, viwanda na kilimo hapa nchini.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jana tarehe 23 Mei, 2017 Ikulu Jijini
Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa
CNMIF na Mbunge wa Bunge la Wananchi wa China Bw. Zhan Xin.
Mhe.
Dkt. Magufuli alisema Tanzania imejiwekea malengo ya kuongeza
uzalishaji wa umeme kutoka Megawatts kati ya 1,500 na 1,800
zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia Megawatts 10,000 na kwamba ili
kufikia malengo hayo wawekezaji wanakaribishwa kuzalisha umeme kwa
kutumia vyanzo vilivyopo kama vile gesi, makaa ya mawe na jua.
“Kwa
hiyo Ndg. Zhang Xin kawaambie wawekezaji wenzako wa China waje
Tanzania, nchini zetu ni ndugu na marafiki wa miaka mingi, itakuwa jambo
jema wakija kuunga mkono juhudi zetu za kujenga viwanda kwa kuzalisha
umeme mwingi na pia kushiriki katika miradi mingine ikiwemo ya ujenzi wa
miundombinu ya reli na barabara” alisema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Magufuli amekutana na Balozi wa Ufaransa hapa nchini Mhe.
Malika Berak ambapo viongozi hao wamezungumzia utekelezaji wa mambo
mbalimbali ya ushirikiano pamoja na miradi ya maendeleo iliyotokana na
makubaliano ya Mkutano wa wafanyabishara wa Tanzania na Ufaransa
uliofanyika hivi karibuni.
Viongozi
wengine ambao leo wamekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais
Magufuli ni Kaimu Balozi wa Uturuki hapa nchini Bw. Yunus Belet na Kaimu
Balozi wa Jamhuri ya Korea Bw. Songwon Shin.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
0 comments:
Chapisha Maoni