1. UTANGULIZI
(i)
Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Gedleyihlekisa Zuma
anatarajiwa kufanya Ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini, kuanzia
tarehe 10 hadi12 Mei 2017, kwa mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(ii)
Ziara hii inafanyika baada ya Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa
Rais Zuma kukutana mjini Addis Ababa, Ethiopia wakati wa Mkutano wa 28
wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
(iii)
Mheshimiwa Rais Zuma anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 10 Mei 2017, jioni na kupokelewa na
mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli.
(iv)
Ziara hii itatoa fursa kwa Viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali
yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa pamoja na kujadili
fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na
biashara. Ujio wa Mheshimiwa Rais Zuma ni fursa nzuri sana ya kuendelea
kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano mazuri naya kihistoria kati ya
nchi zetu mbili.
(v)
Mheshimiwa Rais Zuma anafuatana pia na wafanyabiashara takribani 80.
Hii ni fursa muhimu sana katika kukuza mahusiano ya kibiashara kati ya
Tanzania na Afrika Kusini. Hivyo, tarehe 11 Mei 2017, kutakuwepo na
Kongamano la Wafanyabiashara katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa
Mwalimu Nyerere (JINCC).
(vi)
Ziara ya Mheshimiwa Rais Zuma inaenda sambamba na vikao vya Tume ya
Pamoja ya Marais (Bi-National Commission - BNC) kati ya Tanzania na
Afrika Kusini. Mkutano wa Marais umepangwa kufanyika tarehe 11 Mei,
2017. Mkutano huo utatanguliwa na Kikao cha Mawaziri kitakachofanyika
tarehe 10 Mei, 2017 na kikao cha Makatibu Wakuu kitafanyika tarehe 8 na 9
Mei, 2017.
2.0. RATIBA
(i)
Wakati wa ziara hiyo, tarehe 11 Mei 2017, Mheshimiwa Rais Zuma
atakutana na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli kwa mazungumzo ya
faragha kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa
pande mbili.
(ii) Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa Mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ya ushirikiano.
(iii)
Siku hiyo hiyo, Mheshimiwa Rais Zuma atashiriki chakula cha mchana na
Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini katika Hoteli ya
Hyatt Regency. Pia, Mheshimiwa Rais Zuma na Mheshimiwa Rais Magufuli
watashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini
litakalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
(iv)
Aidha, jioni ya siku hiyo, Mheshimiwa Rais Zumana ujumbe wake
watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu
kwa heshima yake na Mheshimiwa Rais Magufuli.
(v)
Tarehe 12 Mei 2017, Mheshimiwa Rais Zuma anarajiwa kufungua rasmi Jengo
jipya la Ubalozi wa Afrika Kusini nchini pamoja na kutembelea Taasisi
ya Matibabu ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
(vi) Mheshimiwa Rais Zuma na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Afrika Kusini.
3.0. MAHUSIANO BAINA YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI
(i)
Mahusiano ya Tanzania na Afrika Kusini ni mazuri na ni ya muda mrefu
tangu wakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika
Kusini zilizoongozwa na Chama kikongwe cha African National Congress
(ANC). Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika
masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kikanda na hasa
ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Kwa sasa, Afrika Kusini
ni Mwenyekiti wa SADC na Tanzania ni Mweyekiti wa SADC Organ, hatua
inayotoa nafasi ya kushirikiana zaidi.
(ii)
Aidha, ushirikiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa
ukiimarika kila mara kwa Viongozi wakuu kutembeleana na viongozi wa
ngazi za juu Serikalini kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali kwa
ajili ya maendeleo ya nchi zetu mbili. Kama mtakumbuka Julai 2011, Mhe.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alifanya Ziara ya Kiserikali
nchini Afrika Kusini ambayo ndiyo iliyozaa Mkataba wa Ushirikiano wa
Tume ya Marais ambayo ndiyo iliyotuwezesha kukutana leo.
(iii) Uhusiano wa Vyama vya Siasa vya CCM na ANC
Vyama
vya ANC na CCM vina mahusiano mazuri na Viongozi wa vyama hivyo
wamekuwa wakikutana mara kwa mara kwa ajili ya kujadili maeneo
mbalimbali ya ushirikiano kati yao.
(iv) Mikataba ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini
Tanzania
na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali za
kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hadi sasa, Tanzania na Afrika Kusini
tayari zimetia saini Mikataba ya Ushirikiano (MoU) kumi na tano (15),
ambayo inagusa sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, sayansi na
teknolojia, uwekezaji, utamaduni na kilimo.
(v) Ushirikiani katika Utatuzi wa Migogoro katika Kanda
Tanzania
na Afrika Kusini zimeendelea kufanya kazi pamoja katika juhudi za
utatuzi wa migogoro na kuhakikisha kwamba Afrika inakuwa sehemu salama.
Nchi hizi mbili zimeshiriki katika kutatua migogoro nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Sudan Kusini. Tanzania na Afrika
Kusini zote zimechangia Askari katika Brigedi ya Umoja wa Mataifa
inayosimamia Amani na Usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(United Nation Force Intervention Brigade-FIB) kwa lengo la kutuliza
uvunjifu wa amani Mashariki mwa Kongo. Vile vile, nchi hizi mbili kwa
pamoja zimekua zikishirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu ya
mgogoro wa Sudan Kusini.
(vi) Uhusiano katika Nyanja za Uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini
Ø
Uhusiano ya uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa
ukiimarika siku hadi siku. Uhusiano huo mzuri umezidi kuchochea na
kurutubisha ushirikiano wetu wa muda mrefu na wa kihistoria.
Ø
Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zinazochangia idadi kubwa ya
wawekezaji wa kigeni nchini Tanzania. Takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha
kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Centre-TIC)
kimesajili jumla ya miradi 226 kati ya mwaka 1990 hadi 2016. Miradi hiyo
ina thamani ya Dola za Kimarekani zipatazo Milioni 803.15 na imetoa
ajira zipatazo 20,916.
(vii) Uhusiano katika Sekta ya Biashara
Ø
Kiwango cha biashara (volume of trade) imekuwa ikiongezeka kila mwaka.
Mwaka 2007 ilikuwa Tsh Milioni 976,331 na mwaka 2016 ni Tsh
2,402,211.20. Hili ni ongezeko kubwa na linaleta matumaini ya
ushirikiano zaidi.
Ø
Bidhaa ambazo Tanzania inauza nchini Afrika Kusini ni pamoja na maua,
kahawa, wanyama hai, chai, nguo, pamba, vito vya thamani, tumbaku na
mafuta ya kupikia. Bidhaa zinazoagizwa kutoka Afrika Kusini ni pamoja na
maziwa na mazao yote ya maziwa, matunda aina ya apple, mbegu za
mahindi, mafuta ya soya, sukari kwa matumizi ya viwanda, juisi za
matunda, mafuta ya kulainisha mitambo, bidhaa za vileo, Acrylic
polymers, lami, magari, pampu za maji, bidhaa za chuma, vitabu, mashine,
na trela.
(vii) Mchango wa Madawati wa Afrika Kusini kwa Serikali ya Tanzania
Ø
Katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutatua changamoto
mbalimbali za kijamii, kwa kupitia Ubalozi wake hapa nchini, Serikali ya
Afrika Kusini iliweza kuchangia jumla ya madawati 1100 kwa shule za
Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.
Madawati hayo yalikabidhiwa kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI.
Ø
Pamoja na hayo, Serikali ya Afrika Kusini inatarajia kuanzisha programu
mahsusi ya kubadilishana walimu na uzoefu kwa lengo la kuimarisha
ushirikiano na kuinua sekta ya elimu.
4.0. TAARIFA FUPI KUHUSU TUME YA USHIRIKIANO YA MARAIS (BI-NATIONAL COMMISSION) KATI YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI
Sasa naomba niwape taarifa fupi kuhusu Mkutano wa Tume ya Ushirikiano ya Marais
(i)
Tanzania na Afrika Kusini zilisaini Mkataba wa kuanzishwa kwa Tume ya
Ushirikiano ya Marais (Bi-National Commission-BNC) tarehe 19 Julai 2011
kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi. Tume ya Ushirikiano ya
Marais imechukua nafasi ya Tume ya Uchumi ya Pamoja ya Marais
(Presidential Economic Commission-PEC) iliyoanzishwa mwaka 2005. Kama
nilivyosema awali, Mkataba huu ulisainiwa wakati wa ziara ya Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tano, Mhshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
(ii)
Mkataba wa kuanzisha BNC umeainisha maeneo kumi (10) ya ushirikiano
ambayo ni Biashara na Uwekezaji (Trade and Investment), Maendeleo ya
Miundombinu (Infrastructure Development), Kilimo (Agriculture), Elimu,
Sayansi na Teknolojia (Education, Science and Technology), Ulinzi na
Usalama (Defence and Security), Habari, Utamaduni na Michezo
(Infrastructire, Culture and Sports), Afya (Health), Nishati na Madini
(Energy and Minerals) na Maliasili na Utalii (Natural Resources and
Tourism).
(iii)
Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Mashirikiano ya Marais (BNC) unatarajiwa
kufanyika kuanzia leo, tarehe 8 hadi 11 Mei, 2017. Mkutano wa Marais
utatanguliwa na vikao vya Makatibu Wakuu tarehe 8 na 9 Mei, 2017
ukifuatiwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 10 Mei, 2017. Mkutano wa Marais
utafanyika tarehe 11 Mei, 2017 ambapo Mheshimiwa Rais Magufuli na
Mheshimiwa Rais Zuma watakuwa Wenyeviti Wenza wa Mkutano huo.
(iv) Wakati wa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Marais, Mikataba ifuatayo inatarajiwa kutiwa saini:-
(a)
Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Masuala ya Bio Anuwai na
Uhifadhi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Jamhuri ya Afrika Kusini (Memorandum of Understanding between the
Government of the United Republic of Tanzania and the Government of the
Republic of South Africa on Cooperation in the Field of Biodiversity
Conservation and Management);
(b)Hati
ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Maji kati ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini;
na
(c)
Hati ya Makubaliano katika Sekta ya Uchukuzi kati ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini;
(v)
Pia kuna Mikataba mingine inaendelewa kufanyiwa kazi na mara
itakapokamilika, Mawaziri wa sekta husika watasaini. Mikataba hiyo ni
pamoja na wa Sekta ya Utalii, Sekta ya habari, Sekta ya kilimo, sekta ya
afya, niitaje hiyo tu kwa sasa.
(vi)
Tofauti na Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), Tume ya Pamoja ya
Ushirikiano (BNC) inashirikisha Marais wa Nchi mbili ambapo katika JPC
inaishia katika ngazi ya Mawaziri. Ushiriki wa Marais katika Tume ya
Pamoja ya Ushirikiano unatoa uzito wa pekee katika utekelezaji wa maeneo
ya mashirikiano yaliyoafikiwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam,
08 Mei, 2017