HOTELI
yenye hadhi ya nyota tano ya JB Belmont iliyoko jijini hapa, imefungwa
kwa kile kilichoelezwa kuwa imeshindwa kutimiza masharti ya mkataba
baina yake na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
JB
Belmont ambayo inatumiwa zaidi na wageni wa kimataifa wakiwamo viongozi
wa juu wa Serikali na wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa, ilifungwa
jana asubuhi kwa tangazo linaloaminika kubandikwa na watumishi wa NSSF.
Baada
ya kubandikwa kwa tangazo hilo, kuliwekwa kizuizi cha kamba kuwazuia
watu kuingia hotelini jambo lililosababisha taharuki kwa baadhi ya
wateja ambao walibaki wamepigwa butwaa pasipo kujua la kufanya.
Hoteli
hiyo inamilikiwa na familia ya marehemu Justus Buguma ambaye ni raia wa
Uganda, na kabla yake ilikuwa chini ya umiliki wa aliyekuwa Mbunge wa
Vunjo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aloyce Kimaro na ilikuwa
ikifahamika kwa jina la Nyumbani Hotel.
Habari
ambazo zimeifikia Mpekuzi zinaeleza kuwa familia ya Bugumba nayo
imeondolewa kwenye umiliki wa hoteli hiyo na NSSF baada ya kushindwa
kulipa kodi ya pango.
Alipoulizwa
Meneja wa Kanda ya Ziwa wa NSSF, Hamis Fakhi kuhusu kufungwa kwa hoteli
hiyo na wafanyakazi wa taasisi anayoiongoza, alisema jambo hilo ni
kweli. Lakini alikataa kueleza sababu za kufikiwa uamuzi huo.
“Ni
kweli tumefunga hoteli hiyo, lakini sina maelezo mengi ya hilo, nasema
hivyo kwa sababu makubaliano ya mkataba kati ya mmiliki wa hoteli na
NSSF yalifanyikia makao makuu,” alisema Fakhi.
0 comments:
Chapisha Maoni