Waziri
wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe ameipongeza
timu ya Taifa ya Mpira wa miguu(Taifa Stars) kwa kushinda mechi zao
zote mbili za kirafiki dhidi ya Botswana na Burundi.
Ameyasema
hayo mapema hii leo wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini
Dodoma mara baada ya kukaribishwa rasmi Wizarani hapo.
Mwakyembe
amesema kuwa Taifa Stars imempa ukaribisho mzuri katika Wizara hiyo kwa
kumpa zawadi ya ushindi kwa michezo yote miwili iliyofanyika mwishoni
mwa Juma lililopita na katikati mwa Juma hili.
“Nawapongeza
sana wachezaji makocha na viongozi wa Taifa Stars kwa kujituma na
kuipeperusha bendera ya Taifa kwa kushinda mechi zao zote mbili za
kimataifa,”amesema Dkt Mwakyembe.
Aidha
amewahimiza pia watanzania kuendelea kuiunga mkono Timu ya Taifa ya
Mpira wa miguu kwa vijana walio chini ya miaka 17 Serengeti Boys kwa
kuichangia timu hiyo ili iweze kushinda nafasi ya kwenda kushindana
katika kombe la dunia kwa vijana litakalofanyika mwezi Novemba mwaka huu
nchini India.
Hata
hivyo, amelipongeza pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa
kushirikiana na Kamati ya kuhamasisha ushindi kwa Serengeti Boys iliyo
chini ya Charles Hillary kuendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara
yake ili kufanikisha ushindi kwa timu hiyo