Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, jana
baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es salaam, amekiri kuwa anafahamu
kuhusu tukio la uvamizi lililofanyika katika ofisi za Clouds Media
Group.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Waziri Mwakyembe aliyechukua nafasi ya
aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Moses
Nnauye alisema kuwa yeye kwa sasa hawezi kulizungumzia tukio hilo wala
kutoa uamuzi wowote kwa kuwa hajapata ushahidi unaojitegemea.
“Ninachokijua
kuhusu hilo tukio kinatokana na taarifa za vyombo vya habari, taarifa
za magazeti, za redio, za televisheni, na sidhani kama taarifa hizo
zinatosha kwa mimi kutoa uamuzi wowote.”
Ameongeza kuwa bado suala hilo ni la kuchunguzwa zaidi kwani picha inayotolewa ni ya upande mmoja.
“Mlalamikaji
hapa ni Clouds, anayetupa taarifa kuhusu suala hili zima ni Clouds na
wenzake. Kwa hivyo naipata picha hii kwa upande mmoja…”
Aidha
kwa mujibu wa ripoti iliyokuwa imetolewa na kamati iliyoundwa na
aliyekuwa Waziri, Nape Nnauye ilisema kuwa wamesikiliza upande wa
mlalamikaji (Clouds Media Group).
Lakini walipokwenda kwa ajili ya kuusikiliza upande wa mlalamikiwa (RC Paul Makonda) hawakufanikiwa kumpata.
Hii
ni baada ya wao kusubirishwa kwa muda mrefu nje ya ofisi yake na
baadae kuambiwa kuwa Makonda ameondoka na hatoweza kurudi kwa siku hiyo.
Jambo hili liliwafanya wajumbe hao kujiaminisha kuwa Makonda hakuwa
tayari kulizungumzia suala hilo na aliamua kuwatoroka.
Hata
hivyo ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa aliyekuwa Waziri, Nape Nnauye ili
aifikishe katika mamlaka husika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.