Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema matukio yaliyotokea
hivi karibuni likiwamo la aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Nape Nnauye kutolewa bastola, yanaweza kubadili upepo wa
Bunge linalotarajiwa kuketi siku chache zijazo.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, aliwaambia hayo waandishi wa
habari jana waliotaka kufahamu mipango ya chama hicho katika kutumia
mhimili wa Bunge kutokana na uwepo wa matukio ya uvunjaji wa sheria.
Katika hilo, Mnyika alisema Watanzania watarajie Bunge lijalo la Bajeti kuwaka moto.
“Sisi ndio tunaongoza Kambi Rasmi ya Upinzani na ambacho ninaweza
kuwaambia Watanzania ni kwamba watarajie Bunge la Bajeti kuwaka moto
juu ya utendaji wa Serikali. Sasa kuwaka moto namna gani na kuhusu nani
ni masuala ambayo yataonekana katika hatua ya baadaye. Naamini safari
hii haitakuwa wabunge wa Chadema, Ukawa pekee, naamini Bunge litakuwa
kitu kimoja katika kuchukua hatua,” alisema Mnyika.
Chadema Yanunua Ugomvi wa Nape
Katika
hatua nyingine chama hicho kimemtaka Rais Dk. John Magufuli ajitokeze
waziwazi na kusema sababu za kumwondoa aliyekuwa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Pamoja
na hilo, kimetaka Rais Dk. Magufuli aseme iwapo alitoa maelekezo kwa
vyombo vya usalama waliovamia ofisi za Clouds Media Group na yule
aliyemtolea bastola Nape alipokuwa akizuia asizungumze na vyombo vya
habari juzi.
Kauli
hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika,
aliyezungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe,
kuhusu ajenda mbili zilizozungumzwa katika kikao cha Kamati Kuu Maalumu
ya chama hicho kilichoketi Machi 22 na 23, mwaka huu jijini Dar es
Salaam.
“Ni
vyema Rais akaeleza kwa kuwa taarifa za Ikulu hazikufafanua kwanini
amemwondoa Nape. Aeleze waziwazi sababu za kumwondoa Waziri katika
kipindi ambacho taarifa ya kamati iliyoundwa imetolewa ambayo imeeleza
wazi makosa yaliyofanywa na mteule wa rais katika siku chache tu baada
ya kumkingia kifua.
“Imeonekana
matumizi mabaya ya wazi ya watumishi wa vyombo vya usalama ikiwamo
waliovamia kituo cha Clouds kwa bunduki, aliyemtolea Nape bastola, rais
ndiye msimamizi wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama, awaeleze
Watanzania iwapo askari na wanausalama hao wamefanya kazi kwa maelekezo
yake,” alisema Mnyika.
Alisema kama sivyo ni hatua zipi ameelekeza zichukuliwe kwa wahusika wa mambo hayo.
Mnyika
alisema chama hicho kinapinga mwenendo wa matumizi mabaya ya madaraka
ikiwa ni pamoja na kulindwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na
matukio ya hivi karibuni yanayogusa uhuru wa vyombo vya habari ikiwemo
kuvamiwa kwa kituo cha Clouds Media Group pamoja na kitendo cha Nape
kutolewa bastola.
“Uamuzi
wa kumlinda Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa gharama hata ya kumwondoa
Waziri wake ni wazi ni matumizi mabaya ya madaraka. Na matumizi haya
mabaya ya madaraka yamejipenyeza sasa hayamhusu Rais tu pekee bali pia
watendaji wake na vyombo mbalimbali,” alisema Mnyika.
Alisema nchi imeanza kuwa ya kipolisi na matumizi ya vyombo vya dola katika masuala ambayo havipaswi kutumika.
“Tunatoa pole kwa wanahabari kwa mambo hayo pamoja na Nape kwa haya yanayomkuta,” alisema Mnyika.
Alisema haki inapovunjwa mahali popote na kwa raia yeyote, wao kama chama hawasiti kutoa kauli ya kukemea.
Mnyika
aliwataka Watanzania kuungana kupinga mabaya yanayofanywa na Serikali
ili kulinusuru Taifa na hatari zinazoikumba na zitakazoendelea.
“Taarifa
nilizonazo kutoka vyanzo vyangu serikalini ni kwamba, Rais ameamua
kumlinda RC kwa sababu eti Chadema kupitia kwa Mwenyekiti Mbowe ilitoa
msimamo wa kumtaka amchukulie hatua. Watu ndani ya Serikali wanasema
kama atamchukulia hatua eti Rais ataonekana amekidhi matakwa ya
Chadema,” alisema Mnyika.
Alisema
chama chao kina wajibu wa kuikosoa Serikali iwapo haifanyi kazi sawa
sawa na Rais anawajibika kwa wananchi na si Chadema.
Mnyika
alikumbusha kuwa wakati walipotangaza Umoja wa Kupambana na Udikteta
Tanzania (Ukuta), waligusia kauli kuwa; anapoonewa yeyote, unapokuwa
kimya, haki inapovunjwa kwa mtu mmoja ukadhani kwamba haikuhusu, ikaenda
kuvunjwa kwa mtu mwingine ukanyamaza kimya ukadhani kwamba haikuhusu,
ipo siku jambo litakukuta mwenyewe na hakutakuwa na mtu wa kupaza sauti
kwa niaba yako.
Alisema
kauli hii ilionekana kuwahusu upinzani pekee lakini hivi sasa
imejidhihirisha tofauti kutokana na athari zinazojitokeza kwa raia,
vyombo vya habari na baadhi ya wanaCCM.