Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni amemhakikishia Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa yupo
tayari kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta
kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Mhe.
Rais Museveni amesema hayo jana tarehe 26 Februari, 2017 katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakati
akiagana na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli baada ya kumaliza ziara
yake rasmi ya kiserikali ya siku 2 hapa nchini na kurejea Uganda.
“Tulikuwa
na mazungumzo mazuri na Mhe. Rais Magufuli, tumejadili mambo mengi
hususani kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta, tumekubaliana na
Mhe. Rais mambo mengi, na sasa tutakwenda kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa mradi huo” alisema Mhe. Rais Museveni.
Mhe.
Rais Museveni aliwasili hapa nchini juzi asubuhi tarehe 25 Februari,
2017 ambapo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na
jana alitembelea viwanda viwili vinavyomilikiwa na kampuni ya
mfanyabiashara wa Tanzania Bw. Said Salim Bakhresa ambavyo ni kiwanda
cha uzalishaji wa unga wa ngano kilichopo Buguruni na kiwanda cha
uzalishaji wa juisi kilichopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam.
Licha ya kuwekeza nchini Uganda Mfanyabiashara huyo pia amekuwa akipeleka bidhaa zake kwa wingi nchini Uganda.
Pamoja
na Mhe. Rais Magufuli viongozi wengine waliokuwepo wakati wa kumuaga
Mhe. Rais Museveni ni pamoja Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan,
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Viongozi wa Vyombo vya
Ulinzi na Usalama.