Wafanyabiashara sita wamekufa papo hapo
na wengine 12 kujeruhiwa, baada ya lori lililokuwa likiwapeleka mnadani
kuacha njia na kuporomoka kwenye mlima wenye kona nyingi zinazofikia 99
wilayani Lushoto.
Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba zilisema ajali hiyo ilitokea
jana Jumapili jioni katika mlima wenye idadi hizo za kona zinazoanzia
Mng’aro hadi Mlalo wilayani Lushoto, baada ya lori aina ya Mitsubishi
Fuso Canter kuporomoka.
Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema lori hilo
lilikuwa likitokea Kijiji cha Mng’aro kilichopo uwanda wa chini
lilipokuwa likipanda mlima kuelekea Mlalo kwa ajili ya kuwahi soko siku
inayofuata.
Walisema lori hilo lilipofika katikati ya mlima liliacha
njia na kurudi nyuma hatimaye likaporomoka bondeni, huku mizigo
ikiwaangukia watu hao.
Kamanda Wakulyamba aliwataja waliokufa kuwa ni
Jamal Hemed (40), mkazi wa Mlalo, Hassan Rashid (33) wa Nyasa, Bisura
Seif wa Kifungilo, Hadija Said wa Mhelo, Zuena Juma wa Kwedege na Husna
Athumani wa Hemtoye.
Alisema majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa matibabu. Kamanda huyo alisema dereva
wa lori hilo, Nassoro Athumani (25) anatafutwa kwa kuwa alitoroka baada
ya ajali.