Mbunge
wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amesema hatamani kuwa rais bali anataka
siku moja awe Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam juzi alipohojiwa katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Televisheni ya Clouds.
Jibu hilo la Ridhiwani lilitokana na swali aliloulizwa na watangazaji wa kipindi hicho kama ana ndoto za kuwa rais wa nchi.
“Sijawahi kutamani kuwa rais ila muda ukifika natamani kuwa Katibu Mkuu wa CCM,” alisema.
Ridhiwani alisema mafaniko yake hadi hapo alipofikia ni kutokana na mchango wa baba yake ambaye ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
“Malezi
yangu, kuzaliwa na kiongozi kumenisaidia kufika hapa, nisingezaliwa
huko labda ningekuwa mtu tofauti na nilivyo, mzee wangu ana mchango
mkubwa hata jimboni, ananipa changamoto, ananielekeza, ana nafasi ya
kunishauri,” alisema.
Pia
alisema katika kutekeleza sera ya Tanzania ya viwanda, tayari Mkoa wa
Pwani una viwanda 164 vikiwamo vinavyojengwa na vilivyokamilika, huku 84
vikiwa ni vikubwa.
Alisema uwekezaji wa viwanda hivyo umegawanyika katika sehemu mbili, chini ya Sh bilioni tano na ule ulio juu zaidi.
“Sehemu
kubwa ni viwanda vya kuchakata malighafi, kuna vya matunda, marumaru,
nondo, korosho, mabati, saruji na malighafi ya nyumba na vinavyofanya
kazi nikivitaja ni zaidi ya 40,” alisema.
Ridhiwani
alisema jimbo lake na mkoa wote wa Pwani, unafanya jitihada kuhakikisha
bidhaa zilizokuwa zikipatikana China ziweze kupatikana Chalinze ili
kuepuka gharama za usafirishaji.
Alisema
uwekezaji wa kiwanda cha Twyford Tanzania Ceramics kilichotembelewa
wiki hii na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage,
uligharimu Dola za Marekani milioni 158.
Ridhiwani
alisema kiwanda hicho kinachotarajia kukamilika katika kipindi cha
Julai hadi Agosti, kitakuwa na uwezo wa kutoa kontena 28 hadi 30 kwa
siku.
Alisema kupitia kiwanda hicho, wananchi watapata faida kwa kufanya biashara na kuongezeka kwa ajira.
“Kitakuwa
na ajira zaidi ya 2,000 zilizo rasmi, huku zisizo rasmi zikiwa ni zaidi
ya 4,000. Hata hivyo, bado nasisitiza ajira izingatie wazawa kwa sababu
wananchi tayari wanalalamikia upendeleo katika kupeana ajira,
walioajiriwa pale wengi si wakazi wa Chalinze, hata Waziri Mwijage
nilimwambia,” alisema.
Pamoja
na jitihada hizo, alisema utekelezaji wa sera ya Tanzania ya viwanda
unaweza ukakwamishwa kutokana na uwezo wa kutafsiri neno na nia nzuri ya
Rais Dk. John Magufuli.
“Rais
hawezi kujenga viwanda peke yake, wasaidizi tutoe tafsiri sahihi ya nia
yake nzuri, tutekeleze. Sitokubali kumdhalilisha rais, akisimama mwaka
2020 akiulizwa kuwa viwanda viko wapi aseme viko Pwani, atoe mfano
Chalinze,” alisema.