Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza walimu wanaishi mbali na shule wakati
shule zao zina majengo wahame mara moja na warudi kuishi kwenye nyumba
za shule.
Amesema
haifai kuacha walimu waishi mbali na maeneo ya shule kwani hali hiyo
inachangia uchelewaji kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi
au kuwasaidia jioni pale wanapohitajika kufanya hivyo.
Ametoa
agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa, kata
ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa Ijumaa, Desemba 30, 2016 kwenye mkutano
uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.
“Nimeambiwa
kuwa walimu wako wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za
kuishi walimu. Mbona wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini
asubuhi wakati hawana magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia
leo, walimu wote warudi mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa
sababu nyumba zipo,” alisisitiza.
“Uamuzi
wa walimu kuishi jirani na shule ulifikiwa ili mwalimu awepo na
kuwasimamia wanafunzi wakati wakifanya usafi na wakati mwingine aweze
kutoa msaada kwa wanafunzi wanaojisomea jioni pindi wakihitaji msaada au
ufafanuzi,” alisema.
Pia
Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa,
Bw. Andrea Chezue asimamie zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
anapunguza walimu walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za
vijijini ambako kuna upungufu wa walimu.
Alisema
ili kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha elimu nchini, ni vema kila
kijiji kikaweka utaratibu wa kuchangia matofali ili iwe rahisi kuanza
ujenzi wa nyumba za walimu.
Akiwa
katika kijiji cha Mkutingome, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la
Ruangwa aliwahamasisha wakazi wa kijiji hicho wachangie matofali 100
kutoka kila kaya ili yapatikane matofali 40,000 yatakayotumika kujenga
zahanati ya kijiji hicho.
Yeye
aliahidi kuwachangia mabati 150 ambayo kati yake, mabati 100 yatatumika
kuezekea zahanati ya kijiji na mengine 50 yatatumika kukamilisha nyumba
ya Mwalimu ambayo imekaa kwa muda mrefu bila kumaliziwa.
Katika
kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unaanza mara moja, Mkurugenzi wa
kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili
alichangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya
kijiji cha Mkutingome. Nao Umoja wa Wachimbaji Wadogo katika mgodi wa
Namungo ambao uko jirani na kijiji hicho waliahidi kuchangia mifuko 50
ya saruji.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU