Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameguswa na hali ya
uathirika wa matumizi ya dawa za kulevya inayomtesa rapa Chid Benz na
kulazimika kufika nyumbani kwao kuzungumza na mama yake mzazi.
Chidi
Benz anayemiliki tuzo kadhaa za muziki alijikuta amenasa kwenye mtego
wa matumizi ya dawa za kulevya ambao sio tu ulimuondoa kwenye maisha ya
muziki bali pia uliidhoofisha afya yake na kuuondoa kabisa mwili wake wa
‘chuma’.
Kupitia
akaunti yake ya Instagram, Waziri Nchemba ameeleza kusikitishwa na hali
ya Chidi Benz na kutumia nafasi hiyo kuwataka wale wanaojihusisha na
biashara haramu ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani Serikali ya
Awamu ya Tano imeazimia kupambana nao.
Hivi ndivyo alivyoandika:
Nimekutana
na kufanya mazungumzo na mama wa msanii Rashid Makwilo “Chid Benz”
ambaye kwasasa amepatwa na tatizo la Dawa za kulevya.Inasikitisha na
haivumiliki kuona nguvu kazi ya Taifa inapotea huku wauzaji wakinufaika
kwa pesa haramu.Ifahamike wazi vita ya serikali dhidi ya magenge,
wauzaji na wasambazaji wa madawa ya kulevya imeongezeka hasa katika
awamu hii ya tano chini ya Mh.Rais J.P.Magufuli,hivyo anayejihusisha kwa
namna yoyote ni vema akaamua kuachana nayo kabla hajakutwa na mkono wa
dola.
Mbali
ya vyanzo vya taarifa tulivyonavyo,ni wajibu wa kila aliye RAIA MWEMA
kutoa taarifa zitakazo saidia kuangamiza biashara haramu ya madawa ya
kulevya.
Naishukuru familia ya Chid Benz kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha kijana mwenzetu anarejea katika hali yake ya kawaida.
Unaweza kuimba,unaweza kufanikiwa,unaweza kutatua matatizo yako bila kutumia madawa ya kulevya.